2303; Kujiunga na kundi, kukimbia kundi…

Binadamu huwa hatupendi kuona tunafanya kitu kwa kulazimishwa.

Huwa tunapenda kufanya kile ambacho tumechagua wenyewe.

Na hiyo ndiyo sababu kwa nini baadhi ya watu wako tayari kufanya mambo ambayo yana madhara kwao, ili tu kuonesha wamechagua wenyewe.

Tukiielewa saikolojia hii ya binadamu, itatusaidia kwenye mengi sana.

Na moja ya maeneo inaweza kutusaidia ni kuelewa kwa nini watu huwa wanahama kundi moja kwenda jingine.

Iwe ni kwenye dini, siasa na makundi ya aina nyingine.

Mara nyingi watu hufanya hivyo kutafuta uhuru wao, siyo ndani ya kundi, bali kwa maamuzi wanayofanya.

Japo wengi huishia kukosa uhuru zaidi kwenye kundi jipya, lakini hawajali hilo, wanachotaka ni kuona wamechagua wao wenyewe.

Hivyo kama unataka kuwashawishi watu kujiunga na kundi fulani, wafanye waone wanachagua wenyewe kufanya hivyo.
Au wafanye waone kwenye kundi walipo hawakuchagua wenyewe.

Lakini hili pia lina upande mwingine, kwako mwenyewe kujikamata pale unapokimbilia kujiunga na kundi jingine. Unaweza kujipa sababu nyingi utakavyo, ila ya msingi kabisa inaweza kuwa unataka tu kujisikia vizuri kwamba umechagua mwenyewe.

Unapaswa kuwa na tahadhari kwa sababu unakuwa hujajiunga kwa sababu sahihi. Hivyo japo utafurahia kwamba umekuwa huru kuchagua, lakini hakuna kitakachokunufaisha zaidi ya hapo.

Sana sana utakuwa umejipa matumaini hewa, matumaini ambayo hayatafikiwa.

Jisukume kila wakati kujua sababu halisi inayokusukuma kufanya kitu na kisha kupima kama sababu hiyo ni sahihi au la.

Watu wengi hujidanganya kwa sababu zilizo nzuri, ambazo ni tofauti kabisa na sababu halisi.

Kukimbia kundi moja kwenda kujiunga na kundi jingine ambalo halina tofauti sana kwa sababu tu unaona umechagua mwenyewe, hakuna manufaa yoyote kwako kimafanikio.

Kocha.