Kuwa Makini Na Unachotamani, Ukikipata Unaweza Usikihimili.
Dorian Gray, kijana mtanashati na mwenye mwonekano mzuri anachorwa picha yake na mchoraji Basil Hallward.
Mchoraji huyo ana rafiki yake anayeitwa Lord Henry Wotton, ambaye anavutiwa sana na Dorian pamoja na picha yake.
Lord Henry anamweleza Dorian jinsi ujana ulivyo kitu kizuri na muhimu, ila kwa bahati mbaya huwa haudumu.
Ujana huwa unapita haraka na mtu kupoteza mwonekano wake mzuri.
Anamweleza jinsi mwonekano wa picha yake utakavyobaki na uzuri wake, huku yeye akiwa anaupoteza.
Dorian kusikia hayo anafadhaika sana, anaona atapoteza kile anachothamini zaidi na anachokitegemea kwenye maisha.
Hilo linamfanya awe na ombi, kwamba yeye abaki kama alivyo, ila picha ndiyo ibadilike.
Alijua ni kitu ametamani tu na hakujua kama kingetokea kweli.
Lakini kwa namna fulani, namna ambayo hawezi kuielezea, ombi lake linakubalika. Yeye anabaki akiwa kijana huku picha ikibadilika na kuzeeka.
Lakini tangu hapo maisha yake yanakuwa ni ya kila aina ya mikosi.
Picha linaanza kwa msichana aliyempenda sana aliyeitwa Sibyl, msichana aliyekuwa muigizaji na alimchumbia na kumwahidi wataoana.
Lakini anakuja kugundua msichana huyo siyo mahiri kwenye uigizaji kama alivyodhani, hivyo anamuacha, kitu kinachopelekea msichana huyo ajiue.
Kwa kuwa Dorian habadilili, hata uso wake hauoneshi hatia kwa makosa anayofanya. Hivyo hakuna anayemhisi kuhusika na kifo cha Sibyl.
Lakini anapoiangalia picha yake anaona imebadilika, imekuwa na sura ya ukatili, wakati yeye akibaki na sura yake nzuri.
Watu wanazidi kumpenda na kumwamini kwa sura yake na mwonekano wake.
Mabalaa yanaendelea, kila anayejihusisha na Dorian anapatwa na mikosi mbalimbali. Watu wanaanza kumkimbia kwa kuona ana ushawishi mbaya.
Mbaya zaidi ni kwa mwonekano wake ulivyo, hakuna anayedhani ana hatia yoyote, hivyo hata wanaomsema vibaya, wakikutana naye hawaamini waliyokuwa wanayasema.
Mchoraji Basil ambaye pia ni rafiki yake anamtembelea Dorian kutaka kujua tatizo ni nini mpaka amekuwa mtu anayelalamikiwa na wengi.
Dorian inabidi amweleze ukweli kwamba tatizo lilianza na picha aliyomchora.
Basil anaiangalia picha na kuona ikk tofauti kabisa na alivyoichora. Anamtaka Dorian wapige magoti na kuomba ili hali hiyo ibadilike.
Dorian anasema haiwezekani, Basil anasisitiza, Dorian anapatwa hasira na kumuua.
Inabidi atafute njia ya kuficha kifo na mwili wa Basil, anakumbuka rafiki yake wa zamani ambaye ni mkemia, anamwomba amsaidie ila anakataa. Anamhujumu na inabidi akubali.
Dorian anakuja kukutana na kaka wa msichana aliyejiua kwa ajili yake, amepanga kulipa kisasi kwa kumuua. Dorian anakimbilia nje ya mji ili kumwepuka.
Lakini mtu huyo anamfuata huko na kupigwa risasi kwa bahati mbaya akiwa amejificha kwenye pori.
Dorian anazidi kuona maisha yake ni mkosi, lakini anafurahia mtu huyo aliyekuwa anamuwinda kufa.
Baadaye anapata taarifa kwamba Alan, aliyemsaidia kuharibu mwili wa Basil naye amejiua.
Hilo linamuumiza lakini pia linamfurahisha kwa sababu siri yake hakuna mwingine anaijua.
Anaamua sasa awe na maisha mapya, aanze upya ili aondokane na mikosi yote.
Anaona njia ya kufanya hivyo ni kuharibu picha ile.
Anachukua kisu na kuichoma picha, anakufa yeye, picha inarudi kwenye bali yake kama ilivyokuwa wakati inachorwa, huku mwili wa Dorian ukibadilika na kuwa wa mtu mzee.
Hii ni riwaya inayoitwa The Picture of Dorian Gray iliyoandikwa na Oscar Wilde ambayo ina mafunzo mengi mno kwenye maisha.
Na funzo moja ninalopenda tushirikishane hapa ni kuwa makini na yale tunayoomba kwa tamaa zetu binafsi.
Ikitokea yamekubaliwa hata kwa bahati mbaya tu, yanaweza kuharibu maisha yetu kabisa.
Yakubali maisha yako na achana na tamaa, zitayaharibu maisha kuliko manufaa utakayoyapata.
Kusoma uchambuzi kamili wa riwaya hii pamoja na nyingine nzuri tembelea http://www.t.me/somavitabutanzania kisha jiunge.