2305; Vitu vinne vinavyoathiri kipato chako.

Kuna kanuni mbili muhimu sana za kipato ambazo unapaswa kuzizingatia katika safari yako ya utajiri na mafanikio.

Kanuni ya kwanza ni unalipwa kulingana na thamani unayozalisha.

Kanuni ya pili ni hupaswi kuweks ukomo kwenye kipato chako.

Kwa kuzifuata kanuni hizi mbili vizuri, utaweza kuongeza kipato na kufika kwenye utajiri mkubwa.

Maana kama kipato unachoingiza sasa hakitoshelezi, unajua wazi thamani unayotoa ni kidogo, ukitoa thamani zaidi utaongeza kipato.

Na kama unatoa thamani kubwa ila kipato hakiongezeki, utaona wazi kuna namna umeweka ukomo kwenye kipato chako.

Pamoja na kanuni hizo mbili, kuna mambo manne muhimu sana yanayoathiri kipato chako unayopaswa kuyazingatia.

Jambo la kwanza ni upatikanaji (supply) wa thamani unayotoa, kama inapatikana kwa wingi, watu wanakuwa hawapo tayari kulipa sana na ushindani unakuwa mkubwa. Hapo unapaswa kujitofautisha sana ili upatikanaji uwe wa kipekee na kwako tu.

Jambo la pili ni uhitaji (demand) uliopo kwa thamani unayotoa. Kadiri uhitaji unavyokuwa mkubwa, ndivyo watu wanavyokuwa tayari kulipia zaidi na kipato chako kuongezeka. Hapa angalia penge uhitaji mkubwa na kisha uhudumie kwa upekee.

Jambo la tatu ni ubora (quality) wa thamani unayotoa, kadiri thamani inavyokuwa bora ndivyo watu wanakuwa tayari kuilipia na kipato chako kuongezeka zaidi.

Jambo la nne ni wingi (quantity) wa thamani unayotoa, kadiri unavyotoa thamani yako kwa watu wengi zaidi, ndivyo kipato chako kinakua zaidi. Hupaswi kujiwekea kikomo ni watu wangapi unawapa thamani yako. Jenga mfumo wa kuweza kuitoa thamani hiyo kwa watu wengi zaidi iwezekanavyo.

Zingatia kanuni hizo mbili za kipato na mambo hayo manne yanayokiathiri na utaweza kukuza zaidi kipato chako na kufikia lengo la utajiri.

Kocha.