Hivi ndivyo unavyokufa kabla hata hujaanza kuishi…

Rafiki yangu mpendwa,

Vipi kama leo nikakuambia, pamoja na mahangaiko yote ambayo umekuwa unapitia kwenye maisha yako, bado hujaanza kuishi?

Utaona kama nakutania.

Vipi kama nikienda mbali zaidi na kukuambia kuna nafasi kubwa utakufa kabla hata hujaanza kuishi?

Utasema nakuchuria.

Sasa kabla hujafurahia majibu yako na kuendelea na mahangaiko ambayo yatapoteza maisha ambayo hujayaishi, soma kisa hicho hapo chini.

Ivan Ilyich alikuwa ni mwanasheria aliyefika ngazi ya juu kwenye utumishi pamoja na kuwa na kipato kizuri.

Alijaliwa kuwa na mke na watoto, huku akiishi kwenye nyumba nzuri na ya kifahari.

Lakini Ivan alikuwa na tatizo moja, alikuwa na ugonjwa sugu ambao haukuweza kupata tiba.

Alihangaika kwa kila aina ya daktari aliyesikia ni bingwa, lakini matibabu aliyopata hayakusaidia.

Hivyo pamoja na mafanikio aliyopata kwenye maisha, kila siku ilikuwa ni siku ya maumivu kwake, kutokana na ugonjwa aliokuwa nao.

Kwa miaka mingi aliteseka na ugonjwa huo bila ya kupata unafuu wowote.

Mpaka siku anayokaribia kifo chake ndiyo anapata jawabu linalomfanya ajue namna gani aliyapoteza maisha yake.

Akiwa kwenye maumivu makali na amekata tamaa, anajiuliza kwa nini apitie yote hayo, mbona alijitahidi kuyaishi maisha yake vizuri?

Ghafla sauti ndani yake inamuuliza kwani nini hasa unachotaka.
Ivan anajibu anatama kuishi, sauti inamuuliza kuishi maisha ya aina gani.
Ivan anajibu kuishi maisha yake kama alivyokuwa, kwa furaha na utulivu.

Sauti inamuuliza ana mfano gani wa maisha ya furaha ambayo amewahi kuishi.
Ivan anavuta kumbukumbu zake na kugundua kipindi pekee amewahi kuwa na furaha kwenye maisha yake ni alipokuwa mtoto.
Kadiri miaka ilivyokwenda furaha yake ilipungua na akagundua tangu ameoa na hata kupanda vyeo kwenye kazi yake hajawahi kuwa na maisha ya furaha.

Anakumbuka jinsi alivyomchumbia mke wake kabla hajamuoa na walivyopendana. Lakini baada ya kuoana na kupata mtoto maisha yakabadilika sana. Ikawa hakuna tena upendo na maelewano kati yake na mke wake.

Na hapo Ivan akaamua ataweka muda na nguvu zake zote kwenye kazi yake. Kweli anafanya hivyo na kupunguza kabisa muda wa kuwa na familia yake. Kitu kinachopelekea mahusiano na familia yake yasiwe mazuri.

Sauti inamuuliza hayo ndiyo maisha anayotaka kuyarudia?
Ivan anajibu hakuwahi kugundua kwamba japo kwa wengine maisha yake yalikuwa yanapanda, kwake binafsi yalikuwa yanaporomoka, na yameporomoka hasa mpaka kufikia alipo sasa.

Sauti inamwambia sehemu kubwa ya maisha yake ameipoteza kwa kusumbuka na mambo yasiyo na umuhimu wowote. Japo alipanda vyeo na kuheshimiwa na wengine, ndani yake hakujiheshimu mwengewe.

Ivan anagundua hakuyaishi maisha yake kwa namna ilivyokuwa sahihi kwake kuyaishi.
Anagundua aliishi maisha yake kushindana na hata kuwafurahisha wengine na siyo kutimiza kusudi lake.

Mbaya zaidi, hata kwenye dakika za mwisho za uhai wake, familia yake, yaani mke na watoto hawamjali sana.
Wanamuona kama mzigo kwao na mtu pekee anayemjali ni kijana wao wa kazi.

Kisa hiki kinatoka kwenye riwaya inayoitwa THE DEATH OF IVAN ILYICH iliyoandikwa na Leo Tolstoy kuhusu majuto ambayo mtu anayapata wakati wa kufa kwake. Maisha yake yote amepambana kufanikiwa kwa viwango vya dunia, ila yeye binafsi anajisahau, kitu kinachokuja kumuumiza sana mwishoni.

Hivi ndivyo wengi tunavyojisahau kwenye maisha, tunayasahau maisha yetu halisi na kuishi maisha ya wengine.
Ni mpaka pale tunapokikabili kifo ndiyo tunagundua kwamba hatukuwahi kuishi.

Na hapo ndipo tunapokuwa tumekufa kabla hata ya kuishi.

Nina imani baada ya kusoma kisa hiki umebadili majibu ya maswali mawili niliyokuuliza hapo mwanzo.
Na kama umefanya hivyo ni vizuri, kwani ni hatua ya kwanza ya kuhakikisha umeishi kabla hujafa.

Leo jipe muda wa kuyatafakari maisha yako, tangu umepata utambuzi mpaka leo.
Jiulize ni maisha ya nani unaishi, yako au ya kuwafurahisha wengine?

Zikumbuke ndoto zote ambazo umekuwa nazo tangu utotoni, picha ya maisha uliyokuwa nayo, je ndiyo unayoiishi sasa?

Usikimbilie kuhalalisha kwamba yalikuwa mawazo ya utoto na maisha ni magumu hivyo huna namna.

Ukabili ukweli kama ulivyo, kwamba kwa sasa huyaishi maisha yako.
Na una hatua mbili tu za kuchukua,
Moja ni kuanza kuyaishi maisha yako sasa, bila kujali uko kwenye hatua gani.

Mbili ni kuamua kuendelea na maisha ambayo umekuwa nayo na kutokuhangaika na maisha ya ndoto zako.

Ukichagua kuyaishi maisha yako sasa utakufa kwa utulivu, maana utakuwa umeishi kwa mafanikio.

Ukichagua kuendelea na maisha ambayo siyo yako utakufa kwa maumivu na mateso makali, maana hujaishi wewe.

Kila mmoja wetu atakikabili kifo kwa namna yake, lakini majuto makubwa yatakuwa ni kushindwa kuyaishi maisha halisi.

Una nafasi sasa ya kuyabadili maisha yako, itumie vyema.

Kusoma uchambuzi kamili wa kitabu hiki pamoja na vitabu vingine vizuri tembelea http://www.t.me/somavitabutanzania kisha jiunge.

Kocha Dr Makirita Amani.