2308; Mambo muhimu ya kujikumbusha…

Katika safari ya mafanikio, unakabiliana na mambo mengi kiasi kwamba usipojikumbusha yale muhimu unaweza kuyasahau na ukajiingiza kwenye wakati mgumu.

Hapa kuna mambo muhimu ya kujikumbusha katika safari hii ya mapambano.

Usijiwashe moto ili kuwapa joto wengine. Ni muhimu kuwajali wengine na kuweka maslahi yao mbele, lakini usifanye hivyo kwa kujiumiza. Kwani ukishaumia, hutaweza tena kujali maslahi yao.

Hakuna mwenye nguvu ya kukulazimisha ujisikie kwa namna ambayo hutaki kujisikia mwenyewe. Wewe ndiye mwenye maamuzi ya namna gani ujisikie, kwa namna unavyoyatafsiri mambo.

Kwa kila hali usiyoupenda unayokutana nayo, kuna mambo matatu unaweza kufanya, kuibadili, kuikubali au kuachana nayo.

Chochote unachoruhusu mikono yako ishike, kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana, hata kama ni kidogo kiasi gani.

Usitafute muda, tenga muda. Hakuna muda wa ziada utajaokuja kupata kwenye maisha yako, ni kupangilia vizuri huo ulionao.

Wakikulalamikia mbona hawakuoni kijiweni waulize mbona huwaoni maktaba au kwenye maduka ya vitabu. Wakikulalamikia mbona hawakuoni klabu, waulize mbona huwaoni benki.

Wewe siyo kiranja wa dunia, huwezi kuifanya dunia iende kama unavyotaka wewe, kubali dunia ilivyo.

Mtu pekee unayeweza kumbadili hapa duniani ni wewe mwenyewe.

Ushauri ambao hujauomba ni nadra sana ukakusaidia, ushauri ambao hujaombwa ni nadra sana ukapokelewa.

Kocha.