2310; Njia ya kupunguza msongo…
Chanzo kikuu cha msongo wa mawazo huwa ni kuyaruhusu mawazo yazurure yatakavyo.
Unakuwa unafanya kitu kimoja, ila mawazo yako yako kwenye kitu kingine tofauti kabisa.
Kwa mawazo yako kuzurura, yanatengeneza kitu kisichokuwepo, wakati kilicho mbele yako hukofanyi vizuri.
Kinachotokea ni muda unakuwa umeisha, umejipa hofu kubwa na hakuna ulichokamilisha.
Hapo ndipo msongo mkubwa unapokuandama na unaona mambo hayaendi.
Ukiweza kufanyia kazi hilo moja la kudhibiti fikra zako, kwa kuyaweka mawazo yako kwenye kile unachofanya bila ya kuyaruhusu kuzurura, utapunguza sana msongo.
Kwani kutatengeneza yasiyokuwepo na umakini wako wote unapokuwa kwenye kile unachofanya, unakifanya kwa viwango vya juu sana.
Hivyo hata kama kuna vitu huna uhakika navyo kwenye siku zijazo, kwa kujiona umefanya vizuri kilicho mbele yako, unapata matumaini makubwa.
Kwa kila unalofanya, kazana kuyaweka mawazo yako yote pale, lifanye kwa viwango vya juu sana na usiruhusu usumbufu wowote ukutoe kwenye lile unalofanya.
Pia unapofanya, fanya kwa kuwa umechagua kufanya na fanya kwa kuwa unataka kutoa mchango ambao ni bora zaidi.
Kwa kufanya hivi, siyo tu utapunguza msongo, bali pia utakuwa na maisha tulivu na ambayo ni bora pia.
Hili liko ndani ya uwezo wako na unaweza kulianza mara moja.
Chukua hatua.
Kocha.