Kadiri Unavyowabeba Ndivyo Unawafanya Kuwa Hatari Zaidi, Achana Nao.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye maisha huwa tunajaribu kuwabeba kwa kuwasaidia na kuwapa fursa mbalimbali watu wetu wa karibu.

Wapo ambao wanatumia nafasi hizo vizuri na kupiga hatua, kitu kinachotupa faraja sana kuona tumeweza kugusa maisha yao.

Lakini wapo wengine ambao wanashindwa kutumia nafasi hizo, kila tunapojaribu kuwabeba hawabebeki. Unawapa fursa wanazichezea na kuzipoteza.

Jambo hilo linaweza kukuumiza sana, na kukufanya uone bado ni wajibu wako kuhakikisha yule unayemsaidia amefikia pazuri.

Lakini haijalishi una nia nzuri kiasi gani, kuna watu hawabebeki, kuna watu hata ukazane kuwasaidia kiasi gani, msaada wako hauwezi kubadili maisha yao.

Wanakuwa ndivyo walivyo na kitu pekee cha kuwasaidia ni kuacha kuwasaidia. Maana kadiri unavyoendelea kuwasaidia, ndivyo unavyowafanya wawe hatari.

Wanakuwa hatari kwao wenyewe kwa kuwa unawapa fursa ambazo ni kubwa kwao na hivyo zinawaathiri kwa kuwa hawawezi kwenda nazo. Mfano wanazembea kwenye kazi muhimu na hilo linawaweka kwenye hatari.

Pia wanakuwa hatari kwa wengine kwa kuwa fursa unazowapa zinawagusa pia wengine na hivyo chochote wanachofanya kinaathiri wengine.

Wanaweza pia kuwa hatari kwako kwa sababu kadiri unavyowatafutia fursa zaidi na wakaziharibu, ndivyo wanavyochafua jina lako kwa wale ambao wamekuamini kwa muda mrefu.

Hivyo japo inaweza kukuumiza kuona hutawasaidia baadhi ya watu wa karibu kwako, huna namna, hiyo ndiyo njia bora ya kuwasaidia, kuacha kuwasaidia.

Wengine ukiacha kuwabeba na kuwasaidia ndiyo akili zinawakaa sawa na wanapambana na maisha. Wanapojua upo na utabeba mzigo wao hawajihangaishi, ila wakijua haupo tena kubeba mzigo wao, inawabidi wapambane.

Kuna kisa hiki kitoka riwaya ya OF MICE AND MEN ambacho kina funzo kubwa sana kuhusu hili.

George Milton na Lennie Small ni wafanyakazi wa mashambani ambao wamekuwa wanazunguka kutafuta vibarua maeneo mbalimbali.
George ni mwerevu ila hana elimu, Lennie ana mwili mkubwa na nguvu, ila ana tatizo la akili.
Kwa kazi anaweza kufanya vizuri sana kadiri anavyoelekezwa, ila akikasirishwa huwa anafanya mambo yasiyotarajiwa.

George amekuwa akimsaidia Lennie kwenye kila eneo wanalofanya kazi, kumtolea maelezo, kumlinda na hata kumtetea.
Lakini kila mara Lennie amekuwa akiwaingiza kwenye matatizo na wanalazimika kuondoka.

Safari hii wanakimbia kutoka shamba moja ambapo Lennie alishika mwanamke na kutuhumiwa kutaka kumbaka.
Kitu kingine kuhusu Lennie ni kwamba anapenda kushika vitu laini, hivyo kila mara huwa na mtoto wa sungura au hata panya na kumshika nywele zake.

George na Lennie wana ndoto kubwa, wanaamini siku moja watakuwa na shamba lao kubwa ambalo watalima na kufuga na hivyo kuacha kuhangaika kwenye mashamba ya wengine.
George anamsisitizia Lennie ndoto hii mara kwa mara na kumtaka asiisahau, pia awe makini ili asiiharibu.
Lennie anasisitiza wakishakuwa na shamba lao yeye ndiye awahudumie sungura na aruhusiwe kuwashika. George anamwambia kama atatii maagizo anayopewa atapata hilo.

Kitu kingine kuhusu Lennie ni kwamba katika kuwashika sungura au panya, huwa anaishia kuwaua. Maana anawashika kwa muda mrefu na hataki kuwaachia. George amekuwa akimuonya sana kwenye hilo, anaahidi haitajirudia tena, ila inajirudia.

George amewahi kumwambia Lennie kwamba isingekuwa yeye angeshafika mbali sana, maana amekuwa anamrudisha nyuma. Lennie anamwambia kama amekuwa kikwazo kwake basi amuache tu aende zake.
George anamjibu hawezi kumwacha, kwani hatayaweza maisha bila yeye.
Lennie anapata uhakika kwamba George hawezi kuja kumuacha.

Wanapata kazi kwenye ranchi, George anamsihi sana Lennie asifanye kitu chochote cha kijinga. Akichokozwa na mtu asifanye chochote bali aende kwa George. Na pia kama lolote baya litatokea, anamwelekeza sehemu ambayo ataenda kujificha mpaka aje amkute hapo.

Kazi inaanza vizuri, George anaendelea kumlinda Lennie. Lakini kuna changamoto kubwa mbili.
Ya kwanza ni kijana wa bosi ambaye ni mkorofi na hapendi watu wenye miili mikubwa hivyo huwachokoza.
Ya pili ni mke ea kijana huyo wa bosi ambaye anapenda kujenga mazoea na kila mwanaume hapo kwenye ranchi.

George anamtahadharisha sana Lennie kuhusu watu hao wawili, anamwambia hao ni tatizo kubwa akae nao mbali kabisa.
Lennie anamjibu atafanya hivyo.

Siku moja kijana wa bosi anamchokoza Lennie, anakaa kimya, anaendelea kumchokoza na kumpiga, Lennie anashika mkono wake na kuutengua.
Kwa kuwa kijana huyo ndiye alianza kumsumbua, anaambiwa asimsumbue tena.

Maisha yanaendelea, kazi inakwenda vizuri. Katika kuzungumzia ndoto yao, mfanyakazi mwingine anawasikia na kuwaambia amevutiwa na mpango wao. Kama watakuwa tayari atajiunga nao. Anaahidi kuchangia sehemu kubwa ya mtaji kutoka kwenye akiba yake.

Kujiunga kwa mfanyakazi huyo mwingine kunamfanya George aone ndoto iko karibu zaidi. Badala ya kusubiri miaka, sasa watakamilisha kiasi cha fedha wanachohitaji ndani ya mwezi mzima.
Wanamkubalia na wanapata hamasa zaidi ya kukamilisha ndoto yao, huku wakiendelea kupanga mengi watakayofanya kwenye shamba lao.

Siku moja Lennie akiwa kwenye banda la majani, akifanya kile anachopenda, safari hii anabembeleza mtoto wa mbwa, mke wa kijana wa bosi anaingia.
Wapo wawili tu, mwanamke huyo anamweleza jinsi alivyo mpweke hapo kwenye ranchi. Anamweleza ndoto zake ilikuwa ni aje kuwa mwigizaji maarufu lakini sasa anaona zinazima.

Lennie hamjibu kitu, anamwangalia na kuziona nywele zake laini. Anamuomba amshike nywele zake, mwanamke yule anakubali.
Lennie anazishika nywele ambazo ni laini kweli, anazidi kuzishika na kuzivuta, mwanamke huyo anapata maumivu na kupiga kelele.
Hilo linamfanya Lennie ataharuki na kumziba mdomo, mwanamke anazidi kupiga kelele.
Lennie anaendelea kumkaba na kwa nguvu zake anajikuta amenvunja shingo na anakufa.

Lennie haamini kilichotokea, anaondoka na kwenda pale George alimwelekeza aende kama kitu kibaya kitatokea. Anaiba bunduki na kuondoka nayo.
Taarifa za mke wa kijana wa bosi kufa zinajulikana, Lennie haonekani na hivyo kila mtu anajua ndiye amehusika.
Hakuna anayejua ameenda wapi, ila George anajua.
Wote wanatoka kwenda kumtafuta, na kwa kuwa ameondoka na silaha, wanaenda wakiwa wamejipanga vizuri kwa mashambulizi.

George anawaacha na anaenda moja kwa moja alipomwambia Lennie akamsubiri. Anamkuta akiwa amekaa.
Lennie anaeleza kwamba hakukusudia na hajui imetokeaje.
George anamkumbusha ndoto yao kubwa waliyonayo, Lennie anaendelea kusisitiza kulea sungura na kuwashika. George anamwambia ndoto hiyo haiwezekani tena.
George anampiga risasi Lennie na kumuua.
Wengine wanafika pale na kumkuta George akiwa kwenye masikitiko makubwa. Wanamfariji kwamba hakuwa na namna nyingine ya kutatua hilo.

Tumejifunza mengi hapa, jinsi George amekuwa anambeba Lennie ambaye habebeki. Mwisho anagundua kadiri anavyombeba ndivyo anavyokuwa hatari kwa wengine na hivyo kuona hana budi bali kumuua.

Wewe huhitaji kufika hatua hiyo ya kuua, bali unapaswa kujua mapema watu gani ambao hawasaidiki na kuachana nao mapema kabla msaada unaowapa haujawa hatari kwao, kwa wengine na hata kwako pia.

Makala imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani, kupata chambuzi za vitabu vingine vizuri tembelea;
http://www.t.me/somavitabutanzania

Kupata vitabu vizuri vya Kiswahili vya maendeleo binafsi na mafanikio, weka app ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua; http://www.bit.ly/somavitabuapp