2310; U mpweke…

Umewahi kutamani watu wakione kitu kwa namna fulani unavyokiona wewe lakini wanashindwa kufanya hivyo?

Umewahi kuwa na hisia fulani kwenye jambo lakini wengine wakawa na hisia tofauti unayoshindwa kuielewa?

Unapojikuta kwenye hali hiyo usione kama una tatizo, bali tambua ndivyo kila mtu alivyo.

Kila mmoja wetu anaiona dunia kwa namna ya kipekee kabisa kwake, namna ambayo hakuna mwingine anaiona.

Imani ulizojijengea mpaka sasa, mtazamo ulionao, fikra zako na uzoefu uliokutana nao kwenye maisha, vimekujenga wewe kuwa wa kipekee sana.

Hakuna mtu mwingine yeyote anayeweza kuiona dunia kwa namna unavyoiona wewe mwenyewe.

Ni kwa dhana hiyo ndiyo nakuambia kwamba u mpweke na hilo lisikufanye ujisikie vibaya.

Badala yake likufanye kuwa huru, likufanye kuchagua kuyaishi maisha yako na siyo kutaka kuwafurahisha wengine.

Kwa sababu haijalishi utakazana kwa namna gani, huwezi kumridhisha yeyote, kwa sababu huoni dunia kwa namna anavyoiona yeye.

Kila mmoja wetu ni kama amevaa miwani ya rangi na anaiona dunia kwa rangi yake ya kipekee.

Rangi ya miwani hiyo ni imani, mitazamo, fikra na uzoefu ambao mtu amepitia kwenye maisha yake.

Kwa kuzingatia haya, unaweza kuona jinsi gani watu walivyo wagumu kuwaelewa, achilia mbali kuweza kuwadhibiti utakavyo.

U mpweke, tambua hili siyo ujisikie vibaya, bali uwe huru, kwa sababu kila mtu pia ni mpweke kwa namna ya kipekee.

Na pale watu wanaoshindwa kukuelewa, hilo likusumbue, maana hata wewe huwezi kuwaelewa.

Kocha.