Rafiki yangu mpendwa,

Unaweza kuamini tayari tumefika mwezi wa tano kwenye mwaka huu wa 2021?

Mwaka ambao siku siyo nyingi ulikuwa unauita mwaka mpya na ukajiambia kabisa utakuwa mwaka wa mambo mapya!

Sihitaji kukukumbusha jinsi ambayo mengi uliyojipangia kwa mwaka huu umeshaachana nayo, hivyo ndivyo ilivyo kwa wengi.

Leo nimekuja kwako na pendekezo moja, siyo la kurudi kule ulikopanga na kushindwa, bali pendekezo la kujaribu kitu kipya.

Anza kukijaribu kwa siku 30 tu za mwezi huu wa Mei 2021 kisha mwezi unapoisha jifanyie tathmini kuona mabadiliko gani yametokea kwenye maisha yako.

Kama utayapenda mabadiliko hayo endelea na zoezi hilo kwa mwaka mzima, kama hutayapenda achana nalo na rudi kwenye mazoea yako.

Ni siku 30 tu za kufanya jaribio hili na huna cha kupoteza, maana hakuna gharama au kazi ya ziada unayotakiwa kufanya.

JARIBIO LA SIKU 30 LA KUUFANYA MWAKA 2021 KUWA WA MAFANIKIO MAKUBWA.

Mafanikio yetu yanajengwa au kubomolewa na tabia tunazoziishi kila siku.

Siku zetu zinaendeshwa zaidi na tabia ambazo tayari tumeshajijengea.

Ndiyo maana huwa unasikia huwa tunajenga tabia na kisha tabia zinatujenga.

Kwa siku 30 za mwezi Mei 2021, unakwenda kufanya jaribio la kuziishi tabia 10 ninazokwenda kukushirikisha hapa.

Kila siku kamilisha tabia hizo kumi bila kuacha hata siku moja, kisha siku 30 zinapoisha, jifanyie tathmini ya mabadiliko unayoyaona kwenye maisha yako.

TABIA KUMI ZA KUISHI KWA SIKU 30.

1. Kila siku amka mapema, saa moja kabla ya muda wako uliozoea kuamka. Ukishaamka usiangalie simu wala usumbufu wowote, bali anza kwa kufanya sala na/au tahajudi (meditation) kisha chukua notebook yako na andika vipaumbele vya siku hiyo, mambo ambayo utakwenda kufanyia kazi (To Do List). Hayo ndiyo mambo utakayoyapa kipaumbele kwenye siku yako, usifanye mengine kabla hayo hayajaisha.

2. Kila siku fanya mazoezi kwa dakika zisizopungua 30, mazoezi mazuri ni ya kukimbia.

3. Kila siku soma kitabu kwa angalau dakika 30, chagua kitabu chochote unachotaka kusoma, iwe ni cha maendeleo binafsi au maendeleo ya kitaaluma kisha soma kwa angalau dakika 30 kila siku.

4. Kila siku pangilia na dhibiti ulaji wako, punguza kabisa vyakula vya wanga na sukari, kula mboga mboga na matunda kwa wingi, kula nyama kwa kiasi na kunywa maji mengi. Pia dhibiti sana vilevi unavyotumia.

5. Kila siku mpigie simu mteja mmoja ambaye amewahi kunufaika na biashara au kazi yako na ongea naye kuhusiana na biashara au kazi yako na changamoto alizonazo unazoweza kumsaidia kutatua. Pia mpigie mteja tarajiwa mmoja, ambaye bado hajanunua ila ana uhitaji ambao unaweza kumsaidia, mwoneshe jinsi unavyoweza kutatua tatizo lake.

6. Kila siku mpigie simu mtu mmoja wa karibu, ndugu jamaa na marafiki na kuwa na maongezi naye ya kuboresha mahusiano yenu.

7. Kila siku jaribu kitu kipya na ambacho umekuwa unahofia kufanya au umekuwa unaona huwezi, hata kama ni kidogo, fanya. Hii inajenga ujasiri wako na kukuwezesha kuvuka hofu.

8. Kila siku kuwa na fikra chanya, fikra za mafanikio na utajiri mkubwa. Pata muda wa kuwa peke yako na jenga taswira ya ndoto kubwa ulizonazo, jione kama tayari umeshazifikia na amini ni kitu ambacho tayari kipo. Jenga taswira hii kwenye fikra zako na pia kuwa na picha ya ndoto ulizonazo unayotembea nayo au iliyo kwenye simu yako na iangalie mara kwa mara.

9. Kwa kila kipato unachoingiza, iwe ni kwa siku, wiki au mwezi, weka pembeni angalau asilimia kumi ya kipato hicho na iweke mahali ambapo huwezi kuitumia. Fedha ya ziada unayoipata ambayo hukuitegemea, yote iweke kwenye fungu hilo.

10. Kila siku unapoimaliza siku yako, jipe muda wa kutafakari jinsi siku hiyo ilivyokwenda. Jua yapi umefanya vizuri, yapi umekosea na wapi unapaswa kuboresha zaidi. Andika kwenye notebook yako yale uliyojifunza kwenye tafakari hiyo ya jioni. Kwa kufanya tafakari hii kila siku, utaendelea kuwa bora zaidi kwa kila siku mpya unayokwenda kuanza.

Rafiki, ni mambo hayo kumi tu ya kufanya kila siku kwa siku 30 bila kuacha hata siku moja, kisha siku 30 zikiisha jifanyie tathmini, kama matokeo ni mazuri fanya hiyo kuwa sehemu ya maisha yako.

NAFASI YA KUSIMAMIWA KWA KARIBU NA KOCHA.

Rafiki, unaweza kuhamasika hapa na kuona ni kitu rahisi kufanya, lakini utakapoanza kufanya ndiyo utajua siyo rahisi kama inavyoonekana.

Mazoea ambayo tayari unayo yatakuwa kikwazo kikubwa kwako kufanya jaribio hilo, kila mara utashawishika kuacha na kurudi kwenye mazoea.

Hivyo kama unataka kufanya zoezi hili kwa siku 30 bila kuacha, unahitaji usimamizi wa karibu.

Hapa natoa nafasi kwa watu wachache wanaotaka kusimamiwa kwenye hili niwasimamie.

Kupata nafasi hiyo ya kusimamiwa pata kwanza zawadi ya kitabu kipya cha TABIA ZA KITAJIRI, kitabu kinapatikana hapa; http://bit.ly/somavitabuapp

Ukishapata kitabu hicho tuma ujumbe kwenda wasap namba 0717396253 wenye maneno USIMAMIZI WA TABIA ZA KITAJIRI na utapata maelekezo zaidi.

Kwa maulizo yoyote kuhusiana na zoezi hili la siku 30, tuma ujumbe kwenda wasap namba 0717396253.

Zoezi linaanza rasmi Jumapili ya tarehe 02/05/2021 na kumalizika Jumatatu tarehe 31/05/2021. Una siku ya leo kufanya maamuzi na kuingia kwenye zoezi hili muhimu litakalobadili kabisa maisha yako.

Kama kwa kusoma hapa nafsi yako imekuambia hiki ni kitu unachohitaji, basi isikilize, achana na kauli nyingine utakazokuwa unajiambia kwamba huwezi au mambo haya siyo muhimu.

Nafsi yako inakujua vizuri wewe, isikilize na shiriki zoezi hili la siku 30 na utaona mwenyewe jinsi mwaka 2021 unavyoweza kubadilika kwako. Chukua hatua sasa kwa kufuata maelekezo hayo hapo juu.

Rafiki yako,

Kocha Dr Makirita Amani.