2315; Uchoshi Ndiyo Mafanikio…

Kama huwezi kuukubali uchoshi (boredom) na kuishi nao, huwezi kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Mafanikio ni marudio ya muda mrefu ya vitu vinavyoboa.
Wengi hufikiri mafanikio ni matokeo ya tukio moja kubwa la kishujaa, lakini sivyo.

Fikiria kwenye fedha, wengi tunapenda hadithi za mtu aliyetoka kwenye umasikini na kufika kwenye utajiri mkubwa.

Lakini nenda kwenye uhalisia, utajiri ni matokeo ya kurudia rudia vitu vichache na vya kawaida kabisa vinavyoboa.
Kuweka akiba na kuwekeza kwa muda mrefu ndiyo njia pekee ya uhakika ya kufika kwenye utajiri.
Kila anayesoma hadithi za mafanikio anajua hilo, lakini wangapi wanatekeleza?
Hakuna au ni wachache sana, kwa sababu siyo kitu cha kishujaa, siyo cha kusisimua.
Watu huhangaika na njia za mkato zisizo na manufaa kwa sababu tu zinasisimua.

Nenda kwenye afya, ipi njia ya uhakika ya kupunguza uzito na kuwa na afya bora?
Kula kwa afya na kufanya mazoezi mara kwa mara ndiyo jibu.
Lakini njia hiyo haisisimui, njia hiyo haiuziki. Angalia kilichojaa kwenye matangazo ya kupunguza uzito, siyo mazoezi wala ulaji, bali dawa za kunywa ili mtu apunguze uzito.
Dawa hizo huwa hazileti matokeo, lakini zinasisimua, zinauzika na ndizo watu wanakimbizana nazo.

Uchoshi ndiyo njia ya uhakika ya kuelekea kwenye mafanikio katika jambo lolote lile.
Unaweza kuchukua hii kama msingi wako wa kupima fursa mbalimbali zinazokuja mbele yako.
Ukiona ni ya kusisimua na wengi wanahangaika nayo, jua siyo sahihi, achana nazo.

Njia sahihi ni za uchoshi, ambazo hazisisimui na wala haziuziki kirahisi.
Kuanzia kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, matukio yanayoacha manufaa kwetu siyo ya kusisimua yanayotokea mara moja, bali ya uchoshi yanayojirudia mara kwa mara.

Kuwa tayari kwa uchoshi kama unayataka mafanikio. Au hangaika na yanayosisimua na upoteze muda na maisha yako.

Kocha.