2319; Manufaa Mengine Ya Safari Ya Mafanikio…

Mtu mmoja aliyefanikiwa sana aliwahi kuulizwa kama kufika kwenye kilele cha mafanikio kumempa hali ya kuridhika, kama kumekuwa kama alivyotarajia.
Akajibu hapana.

Akaulizwa tena ana ushauri gani kwa wale wanaopambana na safari ya mafanikio, hasa kwa uzoefu wake wa kufikia mafanikio lakini asiridhike na alichokipata?

Mtu huyo alijibu; nawashauri waendelee na mapambano ya safari ya mafanikio, kwa sababu manufaa hayako kwenye kilele, bali yako kwenye safari yenyewe.

Huu ni ushauri muhimu sana ambao kila mtu anauhitaji.
Kufika kwenye kilele cha mafanikio kunaweza kusikupe furaha au kuridhika kama ulivyokuwa unategemea.
Ila mchakato mzima wa safari hiyo, hautakuacha kama ulivyokuwa awali.

Mapambano ya kuelekea kwenye mafanikio yatakubadili mno na yatakuwezesha kufikia na kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yako.

Kama unapambana ili uwe bilionea, manufaa utakayopata siyo kuzipata hizo bilioni, bali mtu unayekuwa katika safari hiyo.
Huwezi kuwa bilionea na ukabaki ulivyo sasa.
Utapitia mabadiliko makubwa sana, ambayo yatakujenga kwa namna ya tofauti kabisa.

Safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa itakufundisha kuwa na nidhamu ya hali ya juu sana. Kwa sababu huwezi kufanikiwa bila nidhamu.

Safari hiyo itakufundisha ujasiri wa kuikabili kila aina ya hofu, kwa sababu bila kukabili hofu huwezi kufanikiwa.

Safari hiyo itakufundisha uvumilivu na ung’ang’anizi, kwa sababu utaanguka na kushindwa mara nyingi, ni kwa kuwa na vitu hivyo ndiyo unaweza kufikia mafanikio makubwa.

Pambana sana na safari hii ya mafanikio, siyo kwa sababu ukishafanikiwa utakuwa na furaha sana, ila kwa sababu utapitia mabadiliko makubwa mpaka unafanikiwa.
Na mabadiliko hayo yatakuacha ukiwa bora mno kuliko ulivyokuwa kabla hujafanikiwa.

Kama unataka kujijua kiundani,
Kama unataka kujua kusudi la maisha yako,
Kama unataka kujua una uwezo mkubwa kiasi gani ndani yako,
Basi ingia kwenye safari ya mafanikio makubwa na usiache maisha yako yote.

Jiwekee malengo makubwa na pambana kuyafanyia kazi mpaka urafiki.
Ukishayafikia usiridhike na kuona umepata kila kitu, badala yake weka malengo makubwa zaidi ya hayo na jisukume kuyafikia pia.
Manufaa unayopata siyo kufikia malengo na kufanikiwa, bali aina ya mtu unayekuwa pale unapofikia malengo na kufanikiwa.

Kama unajiona umekuwa kama mzururaji tu hapa duniani, jiwekee malengo makubwa na pambana nayo kila siku, hata kama hutayafikia, jua hutabaki ulivyo.

Kocha.