2325; Siyo thamani, ni uhaba…

Siyo kila kitu ambacho bei yake inapanda kwa kasi kina thamani ndani yake.
Kuna ambavyo vinapanda bei kwa sababu ya uhaba.

Tunaijua kanuni kuu ya uchumi ambapo nguvu ya soko huamuliwa na vitu viwili; uhitaji (demand) na upatikanaji (supply).

Kitu kikiwa na uhitaji mkubwa, bei yake inakuwa kubwa kwa sababu kila mtu anakitaka. Uhitaju unapokuwa mkubwa, uzalishaji nao unaongezeka na hivyo kupatikana kwa wingi.
Kitu kikipatikaba kwa wingi kuliko uhitaji uliopo, bei yake inashuka.

Sasa kwa kujua nguvu hizi zinazoamua bei, kuna watu huwa wanaweza kucheza na uchumi ili kujinufaisha zaidi.
Wanachofanya ni kudhibiti upatikanaji wa kitu na kuhakikisha kuba uhaba mkubwa. Kisha kutengeneza hadithi ya watu kutaka kitu hicho.

Watu wengi wanapokitaka, huku kukiwa na uhaba, moja kwa moja bei yake inapanda. Bei inapopanda, wanaotaka kunufaika wanaendelea na hadithi za kuwavuta watu zaidi, wakiwaambia wanapitwa na fursa kubwa.

Watu wanavutiwa kununua, siyo kwa sababu wanahitaji kitu hicho, ila kwa sababu wanategemea kitaendelea kupanda bei na watapata thamani kubwa.

Hapo sasa ndipo balaa linatengenezwa. Kadiri wengi wanavyotaka kununua wakitegemea bei ipande ndivyo bei inavyozidi kupanda.

Bei itaenda hivyo mpaka kufika hatua ambayo haiwezi kwenda tena zaidi na hapo bei itaanza kupungua.

Kwa kuwa wengi walinunua wakitegemea bei iendelee kupanda, wanapoona inaanza kushuka, wanakimbilia kuuza.

Hapo sasa mchezo unabadilika, kila mtu anakimbilia kuuza na bei siyo tu inashuka, bali inaporomoka kwa kasi.
Wale walioingia mapema, wakati bei iko chini na wakauza mapema wanakuwa wamenufaika.
Wale waliochelewa kuingia, wakati bei iko juu na wakachelewa kuuza wanapata hasara kubwa.

Epuka sana hali hizi, zinashawishi kweli kuingia maana watu watakuonesha kweli wanapata faida kubwa, lakini ni mtego.
Hata kama unajiambia utajua wakati sahihi wa kutoka ili usipate hasara, siyo rahisi kihivyo, tamaa ikishakukamata utakuja kustuka umeshapoteza.

Kwa kila fursa unayoshawishiwa kuingia kwa sababu inaingiza faida kubwa, angalia chanzo cha faida hiyo kubwa ni nini, je ni thamani kubwa ambayo watu wanaipata au ni uhaba wa kitu hicho.

Kama ni thamani ielewe vizuri na ingia kwa kutoa thamani hiyo kwa namna ya kipekee.
Lakini kama ni uhaba, kaa mbali, lazima kuna watu watapoteza na usidhani wewe ni mjanja kuliko wale waliokushawishi uingie.

Kocha.