2328; Vyanzo viwili vya msongo…
Huwa tunapatwa na msongo au kwa lugha nyingine kuvurugwa pale nambo yanapokwenda tofauti na tulivyotegemea.
Ni rahisi kuona kilichosababisha msongo kwako ni kile kilichotokea. Lakini hiyo siyo kweli.
Kinachokusababishia msongo ni namna unavyopokea kile kilichotokea.
Kwa wengi hupokea kwa aina mbili na hizo ndiyo huwa chanzo kikuu cha msongo.
Moja ni kukataa kukubaliana na kile kilichotokea. Hapa unakataa kile kilichotokea kwa kuona hakikupaswa kutokea na kujaribu kukizuia au kukikataa.
Kwa bahati mbaya sana, kile kinachokuwa kimetokea kinakuwa nje kabisa ya uwezo wetu, hivyo kutokukikubali hakusaidii chochote.
Mbili ni kulazimisha kitu ambacho hakiwezekani.
Pale unapojaribu kulazimisha kitu ambacho hakiwezekani ili tu matokeo yake unavyotaka wewe, unaishia kutengeneza msongo.
Kwa kuwa inakuwa nje ya uwezo wako, unapolazimisha haubadili hali ya kitu, bali unajiumiza mwenyewe.
Unapojikuta kwenye hali ya msongo, kuvurugwa au kutokujisikia vizuri, jiulize maswali haya mawili;
Je ni kitu gani nakataa kukubaliana nacho? Kama kipo kikubali na angalia namna ya maisha kuendelea licha ya kuwepo kwa kitu hicho.
Na je ni nini nalazimisha kitokee? Kama kipo unacholazimisha na kipo nje ya uwezo wako, achana nacho.
Ukiwa mtu wa kukubali yale yaliyo nje ya uwezo wako na kuacha kulazimisha yaliyo nje ya uwezo wako, utapunguza sana msongo na hata mateso kwenye maisha yako.
Maumivu kwenye maisha huwa hayakwepeki, lakini mateso tunayatengeneza wenyewe kwa kutokukubali au kulazimisha yaliyo nje ya uwezo wetu.
Kocha.
Asante kocha
LikeLike
Karibu Alex
LikeLike