2329; Kanuni ya kipato…

Kitapo unachoingiza kinatokaba na kanuni ya kisayansi ambayo ukiielewa na kuifanyia kazi, utaweza kukuza sana kipato chako.

Kanuni hiyo ina vitu vinne muhimu sana.

Kitu cha kwanza ni uhitaji wa kile ambacho unafanya. Kama unachofanya au kuuza ni hitaji la msingi la watu, watasukumwa kuja kulipata hitaji hilo.
Hivyo ili kuongeza kipato chako, fanya kazi au biashara inayogusa mahitaji muhimu ambayo watu wanayo.

Kitu cha pili ni ubora wako kwenye kufanya kile unachofanya. Watu wanapenda kilicho bora na huwa tayari kulipa zaidi ili kupata ubora.
Kuongeza kipato chako, fanya kile unachofanya kwa ubora wa hali ya juu sana, kiasi kwamba watu wanapata thamani kubwa kuliko fedha wanayolipia.

Kitu cha tatu ni ugumu wa kukubadilisha. Kama watu hawawezi kupata mtu mwingine kama wewe, watakuthamini zaidi. Lakini kama wanaweza kukubadilisha kirahisi, kama wanaweza kupata kwa wengine kile unachowapa, hawawezi kukulipa sasa.
Kuongeza kipato chako, jitofautishe kwa namna ambayo huwezi kubadilishwa kirahisi, yaani watu hawawezi kupata kwa wengine kile wanachopata kwako. Kwa kuwa wewe, kufanya kwa ubora na kuwajali wengine, unajijenga kuwa usiyeweza kubadilishwa kirahisi.

Kitu cha nne ni idadi ya watu unaowahudumia. Ukihudumia wengi kipato kinakuwa kikubwa.
Kuongeza kipato chako, wafikie watu wengi zaidi.

Kama kipato unachoingiza hakitoshelezi, iwe umeajiriwa au unafanya biashara, angalia maeneo hayo manne, kuna ambapo hapako sawa.
Ukomo wowote kwenye kipato huwa unaanzia kwenye maeneo hayo manne.

Ukiyafanyia kazi maeneo yote manne, utaweza kuongeza kipato chako kwa viwango vya juu sana.
Hii ni kanuni inayofanya kazi popote na kwa yeyote, ni wewe tu kuielewa na kuanza kuifanyia kazi.

Kocha.