Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala hii ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufika kwenye mafanikio makubwa.
Kwenye makala hii tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kuondoka nyumbani na kwenda kuyaanza maisha yako pale ambapo wazazi wanakukatalia.
Wasomaji wenzetu walioandika kuomba ushauri kwenye hili walikuwa na haya ya kusema;
“Mimi naishi kijijini nakaa na wazazi wao ni wafugaji sasa wananizuia kuodoka kwenda kutafuta maisha kisa mchugaji wa mifugo watakosa. Nina mtaji wa sh laki tano, je nifanyeje ili nitoke home, je biashara gani nikaiazishe mjini, naomba ushauri.” – Dwacy M. M.
“Natishiwa kulaaniwa na wazazi pale ninapowaeleza kuhusu kuondoka
nyumbani kwenda kutafuta maisha yangu nifanyeje?” – White K. K.
Miaka ya nyuma nimewahi kuandika makala niliyoiita ONDOKA NYUMBANI (https://bit.ly/2RWLU7o), kwenye makala hiyo nilieleza kwa nini ni vigumu sana kufanikiwa ukibaki nyumbani ulipozaliwa.
Hata tukiangalia kwenye historia na tamaduni mbalimbali, kuna umri ukishafika unapaswa kutoka pale ulipozoea, kwenda eneo ambalo hujulikani ili uweze kufanya mapambano halisi ya maisha yasiyozuiwa na chochote.
Siyo kwamba huwezi kufanikiwa ukiwa nyumbani, unaweza sana, ila kwa wengi inakuwa kikwazo kikubwa kwa sababu mbalimbali.
Kubwa ikiwa ni mazoea na uhakika wa maisha hata mtu ukishindwa. Kwa kuwa unajua upo nyumbani, huhofii sana kushindwa.
Lakini unapokuwa mbali na nyumbani, unajua hakuna pa kujishika, ni mapambano ufanikiwe au ushindwe huku ukiwa huna pa kujishika.
Changamoto kubwa ya kuondoka nyumbani ni wazazi na watu wa karibu hawatakubaliana na wewe.
Watakuzuia usiondoke nyumbani kwa sababu kubwa mbili.
Moja wataona unakwenda kuteseka hasa ukiwa mbali nao kitu ambacho hawataweza kukusaidia na hivyo watataka ubaki hapo.
Mbili ni wataona wanapoteza msaada wako kwao hasa pale wanapokuwa wanakutegemea kwa namna mbalimbali.
Wazazi na watu wa karibu watakuzuia usiondoke nyumbani kwa nia nzuri kabisa kwao, lakini nia hiyo nzuri haitakuwa na manufaa kwako.
Itakuzuia wewe kujitambua na kukua zaidi ya pale ulipo.
Hivyo kama nafsi yako inakusukuma uondoke nyumbani, unapaswa kufanya hivyo.
Zipo njia kuu mbili za kuondoka nyumbani pale wazazi au watu wa karibu wanapokuzuia.
Njia ya kwanza ni KUOMBA RUHUSA.
Hapa unawaomba wakuruhusu uende ukayatafute maisha nje ya hapo nyumbani.
Ili ombi hili liwe na ushawishi, unapaswa kuwa na mpango kabisa wa wapi unakwenda na unapanga kwenda kufanya nini.
Unaposema unataka kuondoka nyumbani huku huna mpango unaoeleweka, utaonekana hujajipanga vizuri na hakuna atakayekuwa tayari kukuruhusu.
Katika kuomba ruhusa waondoe pia wasiwasi mkubwa walionao kuhusu kuondoka kwako.
Kama wanahofia utaenda kushindwa na uteseke, wape mpango wako wa nini utafanya ikitokea umeshindwa.
Kama watakosa mtu wa kuwasaidia ukiondoka, kuwa na mpango wa hilo kabisa, kama utatafuta mtu mwingine wa kuwasaidia wakati haupo na wewe kugharamia kumlipa mtu huyo.
Kwa kujua kinachowafanya watu wa karibu wasikuruhusu kuondoka nyumbani na ukaandaa mpango mzuri na kuwaeleza, watashawishika kukuruhusu.
Lakini pamoja na kuwapa mpango wako mzuri bado unaweza usieleweke, jibu likabaki ni hapana, usiondoke.
Hapo ndipo unahitaji kutumia njia ya pili.
Njia ya pili ya kuondoka nyumbani pale wazazi au watu wa karibu wanakuzuia ni KUOMBA SAMAHANI.
Kwa kuomba ruhusa na ukanyimwa, huku ndani yako ukiwa na msukumo mkubwa wa kuondoka na kwenda kuanza maisha yako pengine, huna namna zaidi ya kuondoka bila ya ruhusa.
Hapa unaondoka bila ya kupewa ruhusa kwa nia ya kwenda kupambana kutimiza ndoto yako na baadaye kurudi kuja kuomba msamaha kwa ulichofanya.
Watu wanaweza kukunyima ruhusa, lakini hakuna anayeweza kukukatalia msamaha, hasa pale unapokuwa umefanikiwa kwa ulichoenda kufanya.
Unapochagua kutumia njia hii ya pili, lazima uwe umejitoa kweli kweli kupambana mpaka ufanikiwe bila kuangalia nyuma. Maana kwa njia hii utapata lawama nyingi, lakini zote zitasahaulika ukishafanikiwa.
Ukifanikiwa hutahitaji hata kuomba msamaha, wale waliokuwa wanakukatalia watakusamehe wao wenyewe.
Hivyo kama unataka kuondoka nyumbani lakini wazazi au watu wa karibu wanakuzuia, una njia mbili, kuomba ruhusa au kuomba msamaha. Anza na ruhusa, ikishindikana utakuja kuomba msamaha.
Mambo muhimu ya kuzingatia ukitumia njia ya msamaha.
Njia ya msamaha ni njia ngumu, lakini yenye nguvu kubwa kama ukiweza kuitumia vizuri.
Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia unapochagua njia hii;
1. Lazima uwe unajua nini hasa unataka kwenda kufanya au kufikia na una msukumo mkubwa ndani yako kiasi kwamba hupati hata usingizi.
Bila ya shauku na msukumo mkubwa, njia hiyo itakuwa ngumu kwako.
Na kama hujui unachotaka, kama ndiyo kwanza unauliza ukafanye nini basi jua hujawa tayari na wale wanaokuzuia wako sahihi.
Ukiwa unajua kile hasa unachotaka na ukiwa na shauku kubwa ya kukipata, huhitaji hata kuomba ushauri, huhitaji hata kuomba ruhusa, watu watakuruhusu wenyewe kwa sababu wanaiona nguvu kubwa iliyo ndani yako.
2. Mambo hayatakuwa rahisi. Pamoja na kuwa na mpango mzuri unaokwenda kufanyia kazi, bado mambo hayatakwenda kama ulivyopanga.
Utaweka juhudi kubwa lakini matokeo yatakuja tofauti kabisa na matarajio.
Utakutana na changamoto na vikwazo vya kila aina.
Utashindwa na kuanguka, lakini hupaswi kuruhusu chochote kukuzuia kupata kile unachotaka.
Jiandae kupambana hasa, ukijua safari hiyo siyo rahisi. Kuna wakati utatamani kurudi nyumbani kutokana na magumu utakayokuwa unapitia, lakini usikubali kushindwa kwa namna yoyote ile.
Endelea na mapambano mpaka upate kile unachotaka.
3. Lazima uwe tayari kwa lawama, kuchekwa, kukataliwa na kukatishwa tamaa. Watu wa karibu watatumia kila aina ya kitisho kwako unapochagua njia hii. Watakuambia kila aina ya maneno ili tu uachane na mpango wako huo.
Kama hujawa na ngozi ngumu, hutaweza kuhimili hayo na utaachana na mpango wako.
Unahitaji ngozi ngumu kweli kweli, uweze kuyasikia yote hayo na yasikutetereshe. Wazazi wakuambie watakuachia laana lakini hilo lisikutetereshe, maana unajua laana kubwa na itakayokutesa kwenye maisha yako ni kutoishi ndoto zako. Ukishakuwa na mafanikio makubwa, huku unaishi kusudi la maisha yako na kutimiza ndoto zako, hakuna laana inayoweza kukusumbua.
Rasilimali muhimu unazopaswa kuambatana nazo.
Unapochagua njia ya msamaha, lazima uwe na maandalizi sahihi na sehemu kubwa ni kuvunja imani na mitazamo ya zamani na kujijenga upya.
Zifuatazo ni rasilimali za lazima kuwa nazo unapochagua njia hiyo;
1. Kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, hiki kinakuwa mwongozo mkuu wa maisha yako katika kupambana kufika kwenye mafanikio. Utaona jinsi ndani yako ulivyo na nguvu kubwa hata kama wengine hawaioni.
2. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, unahitaji sana uhuru wa kifedha pale unapochagua kuyaishi maisha yako. Kwani bila ya uhuru wa kifedha, huwezi kuwa huru kufanya maamuzi muhimu kwako.
3. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA, hiki kitakusaidia kupata wazo sahihi la biashara kwako, kuweza kuanzisha na kukuza biashara hiyo kwa viwango vya juu na upate mafanikio.
Kupata vitabu hivyo vitatu, wasiliana na namba 0752 977 170
4. Rasilimali ya nne na muhimu kabisa kuwa nayo kwenye hii safari ni kuchagua kuzungukwa na watu sahihi. Maana hii safari itakuwa ndefu na wengi wanaokuzunguka watakuwa wakatishaji tamaa. Usipokuwa na watu sahihi, hutayaweza mapambano.
Ili kuzungukwa na watu sahihi, wenye kiu ya mafanikio na wanaopambana kweli kiasi cha kukupa na wewe hamasa ya kupambana, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni jamii ya kipekee kabisa ya wasaka mafanikio ambayo ukiambatana nayo lazima utafanikiwa.
Kuna nafasi chache sana za kujiunga na jamii hii, tuma ujumbe kwa wasap kwenda namba 0717 396 253 kupata maelekezo.
Fanyia kazi haya uliyojifunza hapa kwenye makala hii ili uweze kuyaishi maisha yako.
Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri
Kocha Dr Makirita Amani.

