2331; Hupati Unachostahili, Bali Unachovumilia…
Huo ndiyo ukweli wa maisha, wanachokupa wengine siyo kile unachkstahili, bali ambacho unakipokea, kukikubali na kukivumilia.
Kujiamini kwako ndiyo kunakuwekea viwango vyako.
Kama hujiamini na uko tayari kupokea viwango vya chini, hivyo ndiyo wengine watakupa.
Kama unajiamini na unakubali viwango vya juu pekee ndivyo utapewa pia.
Kwa dhana hii hii, hupati utajiri unaotaka bali unapata umasikini unaovumilia.
Hiyo ina maana kama utakataa kuvumilia umasikini wa aina yoyote ile, utaishia kupata utajiri mkubwa.
Kama utakataa kwamba hupo tayari kuvumilia vilivyo chini ya viwango vyako na ukajiamini kwenye hilo, huku ukiwa na thamani kubwa unayotoa, watu hawatakuwa na namna, watakupa viwango unavyotaka.
Usimalumu yeyote kwa chochote anachokufanyia kwenye maisha, maana wewe ndiye umemfundisha akufanyie hivyo, kwa sababu anajua utavumilia.
Hata kama mtu amekupiga au kukutukana, ni kwa sababu anajua unaweza kuvumilia hayo.
Utakapokataa kuvumilia yote usiyotaka, watu hawatayafanya tena kwako.
Ubaya ni kwamba ukiwa masikini utalazimika kuvumilia mengi ambayo hukubaliani nayo, hasa yanapofanywa na wenye mamlaka kwako kifedha.
Hivyo kama upo kwenye hali ya aina hiyo, itumie kama hasira ya kufika kwenye utajiri ili uwe huru, uache kuvumilia usiyoyapenda.
Lakini pia kuna makubaliano mbalimbali ya kijamii yanayoweza kukunasa kwenye mtego wa kuvumilia usiyopenda.
Haya usiyaendeleze, yavunje mara, eleza viwango vyako na visimamie hivyo.
Jiamini na jiwekee viwango vyako kisha usipokee wala kuvumilia chochote kilicho chini ya viwango hivyo.
Kocha.