Zama tunazoishi sasa ni zama ngumu mno ambapo mtu usipokuwa na msingi imara utaishia kuanguka vibaya.

Fursa ni nyingi mno, lakini nyingi siyo fursa za kweli.
Fursa hizo zinahamasisha na kutamanisha kwa sababu unaona kabisa wengine wakinufaika nazo.
Kumbe hiyo ni sehemu ya mtego wa kukunasa ili uweze kuingia kwenye fursa hizo na utapeliwe.

Siku chache zilizopita nilipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama msomaji ambaye amekuwa anafuatilia kazi zangu kwa muda mrefu.

Akaendelea kueleza kwamba kuna fursa nzuri angependa kunishirikisha. Ana watu anaofahamiana nao ambao wako nchi za nje na wapo tayari kumfadhili kiasi kikubwa cha fedha (mabilioni) ila hajui afanye nini.

Hivyo anataka tushirikiane, tuandike mradi wa mabilioni na kuwatumia hao watu wake na wapo tayari kutoa fedha hizo kama mradi ukionekana ni mzuri.
Kama tukifanya hivyo na mimi nitakuwa sehemu ya mradi huo na hivyo kunufaika nao.

Baada ya kumsikiliza akijieleza kwenye hayo nilimjibu HAPANA, SITAWEZA. Alionekana kushangaa kwa nini nakataa fursa kubwa hivyo. Nikamwambia atafute watu wengine.

Rafiki, kama kwa kusoma hapo umeshangaa iweje nikatae fursa kubwa ya mabilioni, kama umeiona hiyo ni fursa basi jua wewe ni rahisi sana kutapeliwa.

Kwenye makala hii nitakushirikisha mbinu za kuwajua matapeli na fursa zao za kukunasa ili uepuke kutapeliwa. Kisha mwisho nitakuonesha utapeli ulio kwenye hiyo ‘fursa’ niliyoshirikishwa.

1. Utaingiza pesa bila kufanya kazi.

Kiashiria cha kwanza cha utapeli ni ahadi kwamba utaingiza pesa bila kufanya kazi yoyote ile. Na katika maelezo ya fursa husika, huoni jinsi fedha unayoweka inakwenda kufanya kazi.
Wewe unaambiwa tu weka kiasi fulani na baadaye utavuna faida kubwa. Huelezwi jinsi gani fedha hiyo uliyoweka inakwenda kuzalisha thamani ambayo ndiyo inaleta faida.

Rafiki, hii dunia imekuwepo kwa miaka mingi na katika kipindi chote hicho pamoja na wagunduzi wakubwa waliowahi kuishi, haijawahi kujulikana njia ya kupata pesa bila kufanya kazi, bila kuzalisha thamani kubwa kwa wengine.
Hivyo usidhani wewe una akili sana kuweza kujua fursa za aina hiyo, kama unaambiwa weka tu fedha na uje uvune faida, hapo kuna utapeli.

2. Unaelezwa faida tu, huelezwi hasara.

Kila kazi, biashara na hata uwekezaji huwa una faida na hasara.
Ukipata kazi inayolipa sana inakunyima muda kabisa. Ukipata kazi inayokupa muda haikulipi vizuri.
Huwezi kupanda shamba la mahindi au maharage na mbegu zote ulizoweka zikaota na kuzaa vizuri, haijawahi kutokea hata kwa sayansi ya juu kiasi gani.
Hivyo ndivyo asili ilivyo na ndivyo itaendelea kuwepo. Kuna faida na hasara, kuna kupata na kupoteza. Iko hivyo.

Wanaokuja kwako na fursa za kitapeli wanakueleza kitu kimoja tu, faida. Hadithi zao zimetengenezwa vizuri mno kiasi kwamba ukizisikiliza unaona pesa nje nje.
Umewahi kusikia hadithi za kulima matikiti au mapapai na ukapigiwa hesabu ya heka moja inaingia miche mingapi na kila mche unatoa matunda mangapi na ukapigiwa bei ya kila tunda ukauona utajiri si ndiyo huu?
Nenda shambani ndiyo utakutana na asili isiyokuwa na huruma na ndiyo utaelewa kwamba umetapeliwa.

3. Unaoneshwa mifano ya wachache waliofanikiwa.

Ni vizuri kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa, lakini ni vizuri zaidi kujifunza kutoka kwa walioshindwa.
Maana huwa unafundishwa siri nyingi za mafanikio, ila kubwa kabisa moja umekuwa hufundishwi, ambayo ni; BAHATI.
Ndiyo, kuna wengi ambao wamefanikiwa kwa bahati tu, japo wanaweza wasijue hilo na wakaona ni ujanja au juhudi zao.

Kama watu 100 wanafanya kitu kimoja, kwa namna moja na eneo moja, halafu mmoja akafanikiwa huku 99 wakishindwa, mafanikio ya mtu huyo ni bahati zaidi kuliko juhudi binafsi.

Matapeli huwa wana mifano michache ya watu waliotumia njia zao wakafanikiwa lakini huwa wanaficha mifano ya wengi waliotumia njia zao na wakashindwa vibaya.

Hivyo unapopewa hadithi za waliofanikiwa, usikimbilie kuziamini kwa sababu wanaonekana wazi, bali kazichimbe zaidi na ona kama kuna kitu cha tofauti kimewawezesha kufanikiwa. Angalia wengine wengi ambak pia walikuwa wanafanya kama wao lakini hawajafanikiwa.
Tenganisha bahati na juhudi ili uweze kujua kweli kinacholeta mafanikio.

4. Unapaswa kuchukua hatua haraka la sivyo utaikosa fursa.

Fursa za kitapeli huwa hazitaki upate muda wa kutafakari kitu, hivyo unalazimishwa uchukue hatua haraka la sivyo utaikosa fursa.
Huwa wanafanya hivyo kwa makusudi, wakati wanakuambia kuhusu fursa, wanaibua hisia kali za tamaa ndani yako na tamaa ikishakuwa juu ni rahisi kwako kufanya maamuzi yasiyo sahihi. Hilo ndiyo wanataka.
Wanajua ukipata muda hisia zako zitashuka, utaweza kufikiri kwa usahihi na utaona utapeli ulio kwenye fursa husika.

Richard Branson amewahi kusema fursa ni kama daladala, ukikosa moja jua kuna nyingine inakuja.
Hivyo unapoelezwa kuhusu fursa yoyote ile, jibu lako la kwanza linapaswa kuwa ni wakupe muda uifikirie na kuitafiti kwa kina. Ukiona wanakuambia unapaswa kuchukua hatua sasa au hupaswi kufikiria sana kwa sababu kuna wengine waliofanikiwa tayari wameichukua fursa hiyo, jua hapo kuna utapeli, kaa mbali.

5. Unalazimishwa upate manufaa.

Tangu kugunduliwa kwa fedha na kutumika kama njia ya kubadilishana thamani, hakuna mtu amewahi kutaka mtu mwingine apate fedha kuliko yeye.
Ndiyo maana ukienda kununua kitu na ukaambiwa bei, huwa unauliza kama kuna punguzo.
Ukipewa kazi na kutajiwa malipo, huwa unaomba upewe nyongeza.

Sasa anakuja mtu kwako, ambaye hata siyo ndugu au rafiki yako, ila ana fursa nzuri kwako ya kukuwezesha kupata fedha nyingi.
Unapokuwa humuelewi anaonekana kuumia sana kwa sababu anaona jinsi unavyokosa fedha nyingi.
Na wewe unaamini na kuingia kwenye mtego huo.

Huwa nasema ukiona mtu anakulazimishia sana fursa, jua wewe ndiyo fursa kwake.
Hakuna anayekupenda sana kwenye fedha kiasi cha kuumia pale anapoona huchangamkii fursa.
Swali jingine la kujiuliza kwa hao waleta fursa, je ndugu zao na watu wao wa karibu wameshawapa fursa hiyo ili wanufaike?
Jibu huwa ni hapana, sasa wanawezaje kukupenda wewe mtu wasiyekujua kuliko wanavyowapenda watu wao wa karibu?
Umeshapata jibu hapo, hawawezi kuwatapeli watu wa karibu.

6. Kila mtu anaizungumzia fursa.

Ukishaanza kusikia kila mtu anazungumzia kitu fulani ni fursa nzuri, jua tayari umeshachelewa.
Hata kama fursa ni ya kweli kabisa, kama unaisikia kwa kila mtu, dirisha la kunufaika kwa kiwango kikubwa limeshakupita.
Inakuwa imebaki kuwa fursa kwa wale wapiga debe ambao wanashawishi wengine wajiunge na fursa hiyo maana wao ndiyo watanufaika.
Na hapa ndipo njama kubwa ya utapeli unaofanana na ukweli inapotengenezwa.

Chukua mfano wa fursa kama ya sungura. Mtu anaanza kufuga sungura kwenye mazingira ambayo ufugaji wa sungura siyo wa kiwango kikubwa.
Kwa kuwa upatikanaji ni mdogo, uhitaji unakuwa mkubwa.
Hivyo mtu huyo anaweza kuuza sana kwa sababu hakuna mwingine anayezalisha kama yeye.
Na hapo anaanza kutangaza hiyo ni fursa nzuri na inayolipa.
Anakuonesha wazi kwamba uhitaji upo, soko lipo na faida ni nzuri.
Wewe kwa kuona hivyo unashawishika kuingia kwenye fursa, sasa basi mbegu utanunua kwake, chakula kwake, madawa kwake na ushauri mwingine kutoka kwake.
Mpaka inakuja kufika wakati wa kwenda sokoni, unakuta wenzako wengi walioingia kama wewe nao wanapeleka bidhaa sokoni. Upatikanaji unakuwa mkubwa kuliko uhitaji na bei inapungua sana.
Unajipa moyo ni soko halijakaa vizuri, usichoweza kukiri ni umetapeliwa kwa njama ya hali ya juu kabisa.

Rafiki yangu mpendwa, umepata mwanga mkubwa kuhusu utapeli kwa haya niliyokushirikisha hapa. Haya ni ya msingi kabisa na ambayo huwa yako wazi kwenye kila aina ya utapeli kama utatumia fikra zako badala ya hisia zako kufanya maamuzi.
Ili uepuke kuingia kwenye utapeli mbalimbali, endelea kujifunza na kujijenga kuwa imara.
Hapa kuna vitabu vizuri kwako kujijenga kuwa imara ili usitapeliwe; http://www.bit.ly/somavitabuapp fungua na ujipatie.

Kwa kumalizia, kama bado hujaona utapeli ulio kwenye fursa niliyokuwa nashirikishwa, nikushirikishe hapa kwa ufupi.
Yote niliyoeleza hapo juu utayaona wazi kabisa kwenye kile nilichoshirikisha hapo juu, lakini kuna kitu kimoja ambacho kiliwasha taa nyekundu kwenye fikra zangu na nilipokisikia tu, nikajiambia hapa jibu ni hapana.
Mtu huyo aliponieleza kwamba watu wapo tayari kumpa mabilioni ya fedha ila hajui afanye nini!
Hapa nilijikuta najiuliza yaani watu wapo tayari kumpa mtu mabilioni ya fedha wakati mtu huyo hajui afanye nini? Hicho kitu haijawahi kutokea.

Kutoka kwa rafiki yako mpendwa,
Kocha Dr Makirita Amani.