2342; Muujiza Unaohitaji Sana Kuutumia…
Watu wamekuwa wakiulizwa kama wakipewa nafasi ya kuchagua nguvu moja ya miujiza wangechagua ipi?
Wengi hujibu kuwa na nguvu za kunyanyua vitu vizito au kuweza kuruka hewani.
Hayo yamekuwa siyo majibu sahihi kwa sababu hata ukiwa na nguvu hizo hazina msaada wowote kwako.
Watu wakikuona unakuwa hewani watakuwinda kama wanavyowinda ndege.
Na ni mara ngapi umekwama kwenye maisha yako kwa sababu huwezi kuruka au kunyanyua vitu vizito?
Ukiachana na majibu hayo ya kitoto ambayo hayana manufaa, ipo nguvu moja kubwa ya miujiza iliyo ndani yako ambayo ukiweza kuitumia utafanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Nguvu hiyo ni usomaji wa vitabu.
Hebu fikiria, mtu amefanya kitu kwa miaka 30, amepitia makosa mengi, amejifunza mengi na kisha kuyaweka yote hayo kwenye kitabu ambacho unaweza kusoma ndani ya siku moja!
Kwa kusoma kitabu hicho kwa siku moja, unakuwa umejifunza yale ambayo mwandishi ametumia miaka 30 kujifunza.
Je huoni hiyo ni nguvu ya miujiza mikubwa sana?
Usomaji wa vitabu unaweza kukubadilisha sana.
Unakutoa kuwa mtu wa kawaida na kukupeleka kuwa mtu wa tofauti anayeweza kufanya makubwa sana.
Usomaji unaisafirisha akili yako kwenda maeneo ya mbali au nyakati za mbali wakati mwili uko pale ulipo.
Kama ipo njia ya kusafiri kwenye muda, basi ni kupitia usomaji wa vitabu.
Walioacha alama kubwa hapa duniani siyo kwa sababu waliweza kuruka angani au waliweza kuona ambayo wengine hawawezi kuona.
Bali waliweza kujifunza na kutumia yale waliyojifunza kuyabadili maisha yao.
Nguvu hii tayari iko ndani yako, ni wewe kuiamsha na kuitumia. Tayari unajua kusoma na kupata vitabu ni rahisi mno.
Ni wewe utenge muda na uweke umakini kwenye kujifunza.
Soma, andika uliyojifunza, elewa kwa kina kisha yaweke kwenye maisha yale uliyojifunza.
Na tambua kusoma kitabu mara moja haitoshi, unapaswa kuchagua vitabu unavyojenga navyo maisha yako na kurudia kuvisoma mara nyingi ili kuvielewa kwa kina na kuweza kuyaishi yale unayojifunza kwenye vitabu hivyo.
Unapomsoma mwandishi kwa muda mrefu, anageuka kuwa menta wako, anakuwa kama anasemezana na wewe kupitia maandiko yake.
Na hapo anakuwa menta bora sana kwako. Unapochagua kitabu kuwa menta, anakuwa menta bora kwa sababu unaweza kuongea naye muda wowote na hakuonei wivu ukifanikiwa zaidi.
Soma, hiyo ndiyo nguvu kubwa ya kuweza kufanya miujiza mikubwa kwenye maisha yako.
Kocha.
Asante Sana kocha ni ukweli mtu. Ubarikiwe Sana.
LikeLike
Karibu Tumaini.
LikeLike
Asante Sana kocha, ni ukweli matupu,ubarikiwe Sana.
LikeLike