2344; Chanzo Cha Chuki…

Waambie watu unataka tu ufanye kazi na upate pesa ya kula chakula na kuendesha maisha ya kawaida na watakubaliana na wewe na kukupenda pia.
Waambie watu hao hao kwamba unataka kuwa tajiri mkubwa, uwe na uhuru wa kifedha na kuishi vile unavyotaka, watu hao watakuchukia na kukuona wewe ni mtu mbaya.

Waambie watu unataka kuwa na ajira ya kawaida yenye mshahara kidogo na watakupenda. Waambie unataka kuwa na biashara kubwa, inayokulipa sana na kukupa uhuru watakuchukia.

Waambie watu unataka kuwa raia wa kawaida watakubaliana na wewe na kukupenda. Waambie unataka kuwa raisi wa nchi na watakuchukia, kukupinga na kukukatisha tamaa.

Mpaka hapo umeshaona nini chanzo cha chuki?
Kiko wazi kabisa, ukubwa wa malengo na ndoto.
Watu watakuchukia kulingana na ukubwa wa malengo na ndoto ulizonazo kwa kujilinganisha na wao.

Ukiwa na matajiri na ukasema unataka kuwa tajiri, watafurahi na kukupenda, watakuwa tayari hata kukusaidia. Lakini waambie masikini unataka kuwa tajiri na watakuchukia.

Watu wanakuchukia pale unapokuwa na malengo makubwa kuliko yao na kuonekana unajiamini sana kwenye kuyafikia.
Na chuki hizo siyo kwa ajili yako, bali kwa ajili yao wenyewe.

Wangetamani sana na wao waweze kuwa na ujasiri wa kujiwekea malengo makubwa kama wewe ila hawawezi. Wanajichukia kwa hilo na kurusha chuki zao kwako.

Kwa maana hiyo basi, puuza yeyote anayekuchukia kwa sababu umechagua kuyaishi maisha yako na kufanya makubwa.
Usijisumbue kumshawishi au kumbadili kwa namna yoyote ile, wewe mpuuze tu moja kwa moja na endelea na mapambano yako.

Huwezi kumlazimisha mtu ajipende na kama mtu hajipendi mwenyewe hawezi kukupenda wewe hata iweje.

Watu wanakuchukia siyo kwa sababu yako, bali kwa sababu zao binafsi, kwa kulielewa hili unakuwa huru kuyaishi maisha yako.

Na kama mtu anapata muda na nguvu ya kukuchukia, unafikiri kuna lolote kubwa anapambana nalo kwenye maisha yake?
Sasa kwa nini umruhusu akusumbue?

Kocha.