2348; Kama hawajakuomba, usijisumbue…

Moja ya kitu nimewahi kuandika na wengi wakauliza kwamba hawakuelewa ni hiki; usitoe ushauri kwa mtu ambaye hajakuomba, usipokee ushauri kwa mtu ambaye hujamuomba.

Unaweza kuona kama watu wanahitaji sana ushauri wako, unaona kabisa wanakwenda kukosea na kwa kuwashauri utawasaidia wasiende kuanguka.

Lakini unakumbuka umewahi kufanya hivyo mara nyingi na uliowashauri hawakukusikia, waliendelea kufanya kile ulichowashauri wasifanye na wakakosea na kuumia vibaya.

Ni kawaida yetu binadamu kupenda kujifunza kupitia maumivu, bila maumivu somo huwa haliingii vizuri.
Na mtu hawezi kuomba ushauri kama hajapata maumivu.

Ndiyo maana kuhangaika kwako kuwashauri watu ambao hawajakuomba huwa hakuzai matunda, kwa sababu wanakuwa hawajapata maumivu.

Kwa upande wa kupokea ushauri, kama hujamwomba mtu ushauri na hivyo kumweleza kwa kina kile unachopitia basi ushauri atakaokupa hautakuwa sahihi kwako.
Atakuwa anaona vitu kwa nje na kudhani ameelewa kiasi cha kuweza kukushauri, lakini sivyo.

Na muhimu zaidi, kuna wale wanaokuja kukuomba ushauri huku tayari wameshafanya maamuzi.
Hao wanachotaka ni kujua kama unaunga mkono maamuzi yao au la.

Hawa kwa kuwa wamekuomba, wape ushauri kwa namna iliyo sahihi kwa upande wako na ukiona wanakupinga wakikuambia ushauri wako siyo sahihi, jua tayari walishafanya maamuzi.
Wanajuaje ushauri upi ni sahihi na upi siyo sahihi kama hawajafanya maamuzi tayari?

Kuwa makini sana kwenye eneo hili la ushauri, iwe ni kutoa au kupokea, kwa sababu kwa sehemu kubwa ni maneno matupu yasiyo na msaada kwa yeyote.

Kocha.