2352; Wanaokukosoa Wanakusaidia…
Huwa hatupendi watu watukusoe au kutukatisha tamaa kwenye yale makubwa tunayoamua kufanya.
Tunaona siyo sawa kwa watu kuchagua kutushambulia wakati tunachofanya kinaweza kuwa na manufaa makubwa kwa wengi.
Lakini kama ambavyo tumekuwa tunashirikishana, huwa kuna upande mzuri wa kila jambo. Hata kama kitu unakiona ni kibaya au kigumu kiasi gani, kuna manufaa ambayo kitu hicho kinayo kwako.
Na kwa hili la kukosolewa, manufaa yake ni kupima imani na kujitoa kwako kwenye kitu hicho.
Kama wanaokukosoa wanakukatisha tamaa, maana yake huamini kweli kile unachokifanya au hujajitoa kweli kukifanya.
Kama huwezi kusimamia na kutetea kile unachofanya kwa yeyote anayekikosoa, basi jua siyo kitu sahihi kwako.
Na kama hakuna yeyote anayekupinga au kukukosoa kwa unachofanya, basi jua unafanya kitu cha kawaida sana ambacho kimezoeleka na hivyo jua huwezi kuzalisha matokeo makubwa.
Furahia pale wengine wanapochukua hatua ya kukukosoa, kwanza wanakuwa wamekuonesha unachofanya ni kikubwa na cha tofauti.
Na pili wanakupa nafasi ya kujipima unakiamini na umejitoa kiasi gani katika kufanya kitu hicho.
Ukosoaji wa wengine unakusaidia usipoteze muda kwenye kufanya mambo yasiyo sahihi kwako.
Kocha.