2358; Fanya kwa ubora au usifanye kabisa…
Una nafasi moja tu ya kuishi.
Kila siku inayoisha ni siku unayoipunguza kwenye maisha yako, hutaweza kuipata tena.
Kwa ukomo huo mkubwa ulionao, unapaswa kuwa makini sana na matumizi ya siku zako.
Chochote unachochagua kufanya, kifanye kwa ubora wa hali ya juu kabisa. Kifanye kwa namna ambayo kitakuwa na manufaa makubwa kwa wengine.
Na kama huwezi kukifanya hivyo basi ni bora usikifanye kabisa.
Maana haina manufaa kwa yeyote kwa kufanya kitu hovyo hovyo, kufanya kitu kwa viwango vya juu.
Ni kupoteza muda wako na maisha yako.
Ni kupoteza uwezo mkubwa ulio ndani yako.
Una uwezo wa kuacha alama kubwa hapa duniani kwa kuchagua kuwa na mguso wa tofauti kwenye kila unachofanya.
Weka utu wako ambao ni wa kipekee na tofauti kabisa.
Weka kujali kwako kwa kutanguliza mbele maslahi ya wengine.
Na fanya chochote unachofanya kama vile ndiyo kitu cha mwisho kwako kufanya.
Mafanikio kwenye maisha siyo matokeo ya kitu kimoja kikubwa ambacho mtu unakuwa umefanya. Bali ni matokeo ya vitu vingi vidogo vidogo vilivyofanywa kwa ubora.
Haijalishi unafanya nini, una fursa kubwa ya kufanikiwa kwenye hicho unachofanya kama itakifanya kwa viwango vya juu kabisa.
Punguza mengi unayohangaika nayo na baki na machache utakayoyafanya kwa viwango vya juu sana. Na hayo yatakupa mafanikio pamoja na kukuwezesha kuacha alama kubwa hapa duniani.
Kocha.