Ubora ukiwa ni tabia mafanikio hujipendekeza yenyewe hivyo usiogope kuanza mchakato wa kuwa bora leo katika kile unachokifanya.

Hivi umewahi kukutana na mtu na ukavutiwa jinsi anavyoongea na wateja wake?

Au umeshawahi kukutana na mtu ambaye watu wanamwamini na wanaamini kile anachokisema?

Yani akisema atafanya kazi yako kwa wakati anafanya kweli na huna haja ya kumkumbusha.

Au umewahi kukutana na mtu ambaye watu wako tayari kumkopesha fedha kiasi kikubwa bila hata kuwa na mdhamini?

Hivi umewahi kujiuliza ni kwanini kuna watu wanatafutwa ili waajiriwe au ili wapewe fursa Fulani wakati wengine wanahangaika kutafuta kazi bila kupata kwa muda mrefu? N.k

Siku moja Jonathani Ive mbunifu wa kampuni ya Apple yenye bidhaa za iPod, Smart Phone na iPad alipoulizwa wamewezaje kuendelea kuwa na bidhaa zenye ubora alidai kuwa, “Lengo letu ni rahisi, kubuni na kutengeneza bidhaa bora, kama tukishindwa kutengeneza bidhaa iliyo bora, hatuitengenezi.

Kama wewe ni mfanyakazi, mjasiriamali, au mwanafunzi na kuna mtu au bidhaa au huduma kwako wewe ni bora na unatamani kufikia viwango vyake basi kanuni ni moja “ Usiogope kuanza kuwa bora leo, hata kama hutakuwa leo”.

Kuna baadhi ya watu wanajutia kuwa walianza biashara na wenzao miaka kadhaa na wenzao miaka kadhaa iliyopita lakini kwa kuwa walishindwa kujua kuwa kuna kipindi cha kujifunza na kutengeneza ubora, walipofanya kwa siku chache tu na kuona hakuna mafanikio walighairisha, lakini wenzao walioendelea na kujikusanyia uzoefu leo wamekuwa “ Wabobezi “na sasa ni mamilionea.

Kuna kipindi kirefu cha kupitia kitakachokuandaa kuwa mwenye mafanikio na kama hamasa ya kufanikiwa kwako ni kubwa kuliko hofu ya kushindwa hakika utafanikiwa kwa kuwa hakuna kipindi kigumu kitakachoweza kukukatisha tamaa au kukurudisha nyuma katika harakati za kufukuzia ndoto yako.

Hakuna aliyewahi, kuwa bora kwa mara moja ndio maana Lionel Mesi mchezaji bora wa mpira wa miguu duniani aliwahi kusikika akisema kuwa “ Imenichukua miaka 17 na siku 114 kuwa bora, watu wengi wanadhani kuwa imetokea ghafla usiku mmoja”.

Leo hii ukijaribu kuangalia kuna matoleo mengi ya magari aina ya Merrcedece Benz, Toyota au Nissan. Pia ukijaribu kuangalia hata simu zina matoleo kibao, mfano katika simu aina ya iphone utakuta iphone 6, mara iphone 6s, mara tena ikaja iphone 6cs na kuendelea.

Windows za kompyuta mpaka leo tuna window ten (10) wakati miaka 10 iliyopita haikuwepo.

Hii maana yake ni kuwa kuna maboresho ambayo yanafanyika katika makosa yaliyokuwepo huko nyuma.

Hata Henry Ford alisahau kuweka gia ya nyuma ( reverse gear) katika gari lake la kwanza alioliunda. Lakini leo ukiitazama Ford Ranger unaiona imekamilika na inapendeza na inauzwa zaidi ya milioni 40 za ki tanzania.

Hivyo kitu cha msingi cha kufahamu ni kuwa ubora wa mtu ni mchakato wa kuendelea kupunguza makosa mpaka unakuwa mtaalamu au mbobezi.

Kosa ambalo watu wengi wanalifanya ni uoga wa kuanza mchakato wa wao kuwa bora, wanaogopa kwakuwa wanajua ni mchakato wa muda mrefu, lakini hasara wanayoipata watu hawa ni kubwa kuliko wale wanaokubali kulipa gharama ya kuanza mchakato wa kuwa bora.

Kuwa bora maana yake ni kutafuta uwezo na sifa za kuishi utaalamu katika kile unachokifanya.

Kama wewe ni mfanyabiashara unajijengea uwezo wa kuwasiliana na wateja wako na kuwahudumia kwa kiwango cha juu ambacho hakuna mtu mwingine anayeweza kuwahudumia kama wewe.

Ukisema saa tano utapiga simu kwa mteja- unapiga, ukisema mzigo utafika kesho unahakikisha umefika, mpaka watu wasiokujua wanapoelezwa kuhusu wewe, wawe na imani ya kufanya biashara na wewe bila kuwa na mashaka yoyote.

Hivyo usisubiri ukidhani kuwa matatizo na changamoto ulizo nazo zitaisha siku moja, bali kubali kuanza safari ya kuwa bora leo. Acha visingizio, acha tabia zinazokuondoa katika ubora na jenga tabia zinazokuondoa katika ubora na jenga tabia zitakazokufanya uwe bora ili miaka mitano ijayo tuone toleo lako bora (The Best Version Of You).

 Haya Ni Mambo Mawili (2) Yanayotokea Kwa Kufanya Mambo Bila Ubora;-

Unajipotezea Fursa.

Huduma au bidhaa unayotoa kwa viwango vya kawaida bila ubora, haiwezi kuonekana kirahisi kwakuwa kila mtu anapenda kupata huduma ama bidhaa iliyo bora hata Yule asiye na kipato kikubwa, hivyo macho ya watu wote wanaotafuta huduma au bidhaa hujikita katika kutafuta bidhaa au huduma zilizo bora.

Watu wanaofanya mambo kwa ubora wa chini huishia kukosa wateja au kupata wateja wa hali ya chini ambao hawawezi kununua bidhaa au huduma kwa bei kubwa hivyo inapelekea faida kuwa ndogo pia.

Unaongeza Ushindani.

Watu wengi duniani ni watu wanaofanya mambo katika viwango vya chini na vya kawaida, watu wanaofanya mambo kwa ubora unaokubalika wako wachache sana, kwahiyo unapofanya mambo kwa kawaida ujue washindani wako ni wengi sana, ila ukiamua kujitofautisha kwa kuwa bora unapunguza washindani (competitors) na unajipatia nafasi nzuri ya kuwa na wateja wengi au kuuza bidhaa/ huduma yako kwa bei ghali mno.

Angalia bidhaa za kampuni ya Apple iwe ni kompyuta au simu, huwezi kukuta zikiuzwa bei rahisi, hii ni kutokana na ubora walio nao. Kuanzia leo kwa chochote unachokifanya jitahidi kujiuliza, je ninafanya kwa ubora unaohitajika?

Ukweli mchungu ni kwamba huwezi kuwa bora na mbobezi kwenye kile unachofanya kama hupendi kujifunza na kusoma vitabu vitakavyokusaidia kuharakisha safari yako ya kuwa mbobezi.

Rafiki yangu ata wewe leo hii unaweza kuharakisha safari yako ya ubobezi kwenye kile unachofanya  kwa kusoma vitabu mbalimbali ambavyo vinapatikana hapa (www.amkamtanzania.com/vitabu).

Unavyozidi kuwa na maarifa sahihi kwenye kile unachokifanya moja kwa moja utakuwa bora na utaharakisha safari yako ya kuwa mbobezi.

Tuendelee Kujifunza hapa (www.amkamtanzania.com) ,kila siku.