2359; Jipe Zawadi Ya Umakini…
Kama kuna zawadi bora kabisa unayoweza kujipa kwenye maisha yako, ni kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya.
Kadiri unavyoweka umakini wako kwenye kile unachofanya, ndivyo unavyoweza kukifanya kwa ubora wa hali ya juu sana.
Na kama hiyo haitoshi, inakupunguzia kuhofia mambo yasiyo na umuhimu wowote kwako.
Iko hivi, akili zetu binadamu zina uwezo mkubwa sana wa kujenga taswira yoyote ile.
Akili inapokuwa tupu, inaishia kutengeneza taswira za kushindwa, kitu kinachokujengea hofu kubwa.
Unapoweka umakini mkubwa kwenye kile unachofanya, huipi nafasi akili yako kutengeneza taswira hizo za kutisha.
Akili kubwa huwa inafunguka pale unapoweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya bila kuruhusu usumbufu wowote ule ukuondoke kwenye kile unachofanya.
Imekuwa vigumu kwa watu kufungua akili zao kubwa zama hizi kwa sababu kabla umakini haujakolea kwenye kazi, tayari anakuwa ameshahamisha mawazo na kwenda kwenye simu au mitandao ya kijamii.
Tunawaona wagunduzi wa zamani kama watu waliokuwa na akili kubwa, lakini ukweli ni walikuwa na akili kama tulizonazo sasa, ila waliweka umakini mkubwa.
Huwa kuna taarifa kwamba Newton aligundua nguvu ya mvutano ya dunia akiwa amekaa chini ya mti na kuona tunda likianguka chini. Nimewahi kuandika kama ingekuwa zama hizi, Newton asingeweza kugundua nguvu hiyo kwa sababu macho yake yangekuwa bize kwenye simu na hivyo asingeona tunda likianguka na kujihoji maswali muhimu.
Nimewahi kumsikia mhamasishaji mkubwa kwenye mtandao wa YouTube ambaye amekuwa akisema kwa miaka 12 alikuwa akifanya kazi masaa 18 kwa siku kwenye biashara ya baba yake.
Anakiri wazi kwamba kama kipindi hicho mitandao ya kijamii ingekuwepo, ana uhakika asingefikia mafaniko aliyofikia sasa.
Anasema umakini wake wote ungenda kwenye mitandao hiyo na asingeweza kufanya makubwa.
Tunazidi kuona hapo ni jinsi gani umakini ulivyo zawadi bora kabisa unayoweza kujipa, hasa kwenye zama hizi za usumbufu wa kila aina.
Tenga muda wa kutekeleza majukumu yako muhimu, jitenge na kila aina ya usumbufu kwenye muda huo na weka umakini wako wote kwenye kile unachofanya.
Utashangaa jinsi akili kubwa itakavyofunguka kwako na kupata majawabu ambayo huwezi kuelezea umeyapataje.
Kocha.