2371; Kubwa na Bora…

Kuna mitazamo miwili kinzani kwenye mafanikio.
Upo mtazamo wa kujenga kitu ambacho ni bora sana kwa wale wanaolengwa.
Na upo mtazamo wa kujenga kitu ambacho ni kikubwa na kuwafikia wengi.

Mitazamo hii huwa inakinzana kwa sababu watu wanaamini hivyo viwili haviwezi kuwa pamoja.
Kwamba kikiwa bora hakiwezi kuwa kikubwa na kikiwa kikubwa kinapoteza ubora.

Kwa kuwa sisi tunatengeneza mafanikio ya tofauti kabisa, tunapaswa kuamini vyote viwili vinawezekana na kujenga mafanikio yenye hivyo viwili, kubwa na bora.

Lakini tunaanza na ubora, kufanya kile kilicho bora kabisa kwa namna ambayo mtu hawezi kupata mahali pengine.
Halafu tunaenda kwenye ukubwa, huku tukilinda ubora ambao tumeshautengeneza.

Hili siyo rahisi na limewashinda wengi, linahitaji kujitoa kweli na kuwa tayari kusema hapana kwenye mengi.

Mfano wakati unaanzia chini na kujenga ubora, unaweza kumkubalia kila mtu.
Lakini kadiri unavyokua, ili kulinda ubora inabidi uwakatalie wengi.
Hapo hawatakuelewa, wataona umekua na sasa unaringa au unawatenga.
Lakini hupaswi kuacha kusimamia kilicho sahihi kwa sababu ya watu wanavyotaka uwe.

Wewe unahitaji kujenga kitu kikubwa na ambacho ni bora, unahitaji kuendelea kukua kwa viwango na ubora.
Kila wakati ujiulize wapi unaweza kuboresha zaidi.
Uangalie hitaji au tatizo lipi unaweza kulitatua, kwa ukubwa na ubora zaidi.

Usifikiria hiki au kile, bali fikiria vyote kwa pamoja.
Ukubwa na ubora vinapaswa kwenda pamoja ili uweze kupata mafanikio makubwa na yanayodumu.

Kama bado hujafika unakotaka, una maswali mawili tu ya kujiuliza;
Moja, wapi nahitaji kuboresha zaidi.
Mbili, wapi nahitaji kukua zaidi.
Ukifanyia kazi maeneo hayo mawili, huwezi kubaki pale ulipo sasa.

Na katika maisha yako yote, hata kama umefanikiwa kwa viwango gani, endelea kujiuliza maswali hayo mawili.
Usije hata siku moja ukaona umeshafika kwenye kilele cha mafanikio na umeshamaliza kila kitu.
Tambua kila wakati kuna mahali unaweza kuboresha zaidi na kuna mahali unaweza kukuza zaidi.

Haijalishi biashara au huduma yako ni bora kiasi gani, kuna mteja ana malalamiko, hapo ni mahali pa kuboresha.
Haijalishi biashara yako imekuwa kubwa kiasi gani, kuna mteja ambaye angeweza kunufaika nayo ila bado hajaijua, hiyo ni fursa ya ukuaji.

Usiridhike wala kubweteka, endelea kuweka juhudi kwenye maeneo hayo mawili kila siku na utapiga hatua kubwa zaidi.
Usifikirie kwa kujiwekea ukomo, bali kuwa wazi kwa ukuaji zaidi.

Kocha.