2372; Tunategemeana Sana…
Pata picha hii,
Kumetokea janga kubwa kabisa duniani na watu wote wamekufa isipokuwa wewe mwenyewe tu ndiye umebaki hai.
Kwa kifupi wewe ndiye unayeimiliki dunia, iko wazi kwamba utakuwa ndiye tajiri namba moja na pekee kwenye hii dunia, maana unamiliki kila kitu.
Sasa hebu pata picha unawezaje kutumia utajiri huo?
Unazo ndege lakini huwezi kuziendesha. Haya giza likiingia huwezi kuwasha taa maana hakuna anayeendesha mitambo inayozalisha umeme.
Unaweza kuwa na chakula cha kutosha kula kwa muda, lakini kikiisha unaweza hata ukafa njaa, maana hutaweza kuzalisha chakula chote unachohitaji.
Kwa kifupi utakuwa na kila kitu, ila kwa sehemu kubwa hutaweza kutumia vile ulivyonavyo.
Mfano huo rahisi unaonesha ni jinsi gani tunategemeana sana kwenye maisha.
Hili ni jambo rahisi kusahau, kwa sababu mambo yanapokuwa yanaenda tunachukulia poa.
Lakini siku mambo hayaendi tulivyozoea, ndiyo tunagundua umuhimu wa wengine.
Huwa kuna kichekesho huwa nakiona mtandaoni, kichekesho kinaeleza; watu huwa hawajui jinsi gani maamuzi yao yanaathiri maisha ya wengine, ni siku ya tatu sasa mama muuza mihogo hajafungua.
Wengi huchukulia hicho ni kichekesho tu, lakini ndani yake kimebeba ujumbe mzito sana, kwamba kila maamuzi unayofanya, hata kama ni madogo kiasi gani, yanawaathiri wengine.
Kwa kujua hili, tunapaswa kuwafikiria wengine pale tunapofanya maamuzi yoyote yale na siyo kujifikiria sisi wenyewe tu.
Tunategemeana sana, tukitambua na kuthamini hili, tutaweza kupata kile tunachotaka kwa kuwapa wengine kile wanachotaka.
Kocha.
Nilipopata changamoto ya kiafya ndiyo nililijua hilo.
Kuna biashara yangu moja inaniingizia kipato kidogo sana
Lakini kwa sababu ina tegemewa na watu wengi nimeamua kuivumilia badala ya kuivunja
LikeLike
Asante Kasanda kwa ushuhuda huu.
Siyo rahisi kuona kitu kama hicho pale mambo yanapokuwa vizuri hasa kwa upande wako. Lakini unapopata nafasi ya kuangalia kwa kina, unajionea wazi.
LikeLike