2374; Mrejesho Ni Zawadi…

Huwa kuna kauli kwamba zawadi ni zawadi, hakuna ndogo wala kubwa. Ukipewa zawadi unapaswa kushukuru.

Moja ya zawadi ambayo mtu yeyote anaweza kukupa ni mrejesho kwenye kile unachofanya.

Unapompata mtu anayeelewa kile unachofanya, na akawa tayari kukupa mrejesho kwenye kile unachofanya, hiyo ni zawadi ya kipekee.

Ni zawadi kwa sababu anakuwezesha kuona kile ambacho wewe mwenyewe huwezi kukiona.
Kila mmoja wetu ana upofu inapokuja kwenye madhaifu yake mwenyewe.

Siyo rahisi wewe mwenyewe kuyajua na kuyaona madhaifu yako. Kuna vitu kwako utaona ni kawaida lakini kwa wengine havijakaa vizuri.

Hivyo unapoipata zawadi hii, ya mtu kukupa mrejesho kwenye kile unachofanya, itumie vizuri. Ifanye kuwa sehemu ya kuona kile ambacho hukioni.

Katika zawadi hii unapaswa kuwa makini na madhaifu ya aina mbili.

Moja ni watu wanaokukubali sana na hawataki kukuumiza. Hawa watakuambia vitu unavyotaka kusikia tu na hivyo hutajifunza kwa kuwa huuoni ukweli.

Mbili ni watu wasiojua kwa kina kile unachofanya na wanaamua tu kukukatisha tamaa. Hawa hawajali chochote na hata wakishakupa mrejesho wao, hawakumbuki hata walichokuambia.

Tengeneza mfumo mzuri wa kupata mrejesho na maoni kutoka kwa watu sahihi, ili uweze kuuona ukweli na kuchukua hatua sahihi.

Kama upo kwenye biashara, hakikisha una njia ya kupata mrejesho na maoni ya wateja wako. Hayo yatakusaidia kujua nini hasa wanachotaka na njia ipi bora ya kuwahudumia.

Pia tambua watu wanachukua hatua ya kujasiri kukupa mrejesho na maoni yao, hasa pale yanapokuwa siyo mazuri.
Ukiwa mtu wa kukatisha tamaa wale wanaojitoa kukupa mrejesho na maoni yao, utakuwa unajinyima zawadi hiyo nzuri na utashindwa kupiga hatua kubwa kwenye kile unachofanya.

Kocha.