2394; Siyo Kweli…
Zoezi rahisi la kufanya leo.
Andika kile unachokitaka sana kwenye maisha yako lakini bado hujakipata.
Kisha orodhesha sababu zote kwa nini mpaka sasa hujakipata.
Mbele ya kila sababu, andika ni uongo.
Halafu tafuta walioweza kupata kitu hicho wakiwa na sababu unazojipa wewe.
Kama unajiambia hujaanzisha biashara kwa sababu huna mtaji au muda, jiambie siyo kweli. Halafu angalia wale walioweza kuanzisha biashara bila ya mtaji na huku wakiwa hawana muda.
Uko hapo ulipo sasa kwa sababu unakubaliana napo, kwa sababu uko tayari kupavumilia.
Kama ungekuwa hukubaliani na ulipo, kama ungekuwa huwezi kupavumilia, usingekuwa hapo.
Nimewahi kutumia mfano wa mtu mmoja aliyesikia mbwa wa jirani yake akilia kwa uchungu sana.
Alishindwa kuvumilia na akaamua kwenda kwa jirani huyo, akamkuta jirani anasoma gazeti huku pembeni yake mbwa akiwa akalia moto.
Jirani akashangazwa na kumuuliza mbona mbwa wako analia kwa maumivu na wewe humtoi kwenye huo moto? Jirani huyo akamjibu, huyo mbwa hajafungwa kamba, yuko huru kuondoka hapo alipokaa, ila kwa kuwa anaweza kuvumilia hali hiyo, anaendelea kukaa hapo.
Jiulize kwenye maisha yako ni moto gani umekalia, ambao unaulalamikia sana lakini huchukui hatua ya kuuacha?
Je ni kazi ambayo umekuwa nayo kwa muda mrefu? Au mahusiano ambayo unajua kabisa ni kikwazo kwako?
Kuna mambo unayalalamikia sana kwenye maisha wakati unachohitaji ni kuamua mara moja kuachana nayo au kuyabadili.
Kama unataka kuendelea kujidanganya na kujifariji fanya hivyo, lakini kama unataka kuukabili ukweli utakaokuwezesha kufanikiwa, tambua sababu nyingi unazojipa siyo za kweli.
Kocha.