Rafiki yangu mpendwa,
Kila kitu kwenye maisha huwa kina majira yake.
Kama ambavyo mwaka hupitia majira mbalimbali, kama masika, kiangazi, kipupwe na vuli, ndivyo pia biashara zinavyopitia majira mbalimbali.
Kama ambavyo siku hubadilika kwenye usiku na mchana, ndivyo pia biashara zetu hubadilika.
Walio kwenye biashara kwa muda na wakafanikiwa, wanayajua vizuri majira ya biashara zao na mambo ya kufanya kwenye kila majira ili biashara iendelee kufanikiwa.
Ambao hawafanikiwi kwenye biashara ni wale wasioyajua majira ya biashara zao na hivyo kufanya tu kwa mazoea bila kujali wanapitia kipindi gani.
Kama ambavyo mchana tunafanya kazi tukijua usiku unakuja na usiku tunalala tukijua patakucha tena, ndivyo unavyopaswa kuyajua majira mbalimbali ya biashara yako na hatua za kuchukua.

Hapa tutajifunza vipindi vinne muhimu vya biashara na mambo ya kuzingatia kwenye kila kipindi ili biashara iweze kukua na ufanikiwe.
Kipindi cha kwanza; Biashara changa.
Kila biashara huwa inaanzia kwenye uchanga.
Hii ni miaka miwili ya kwanza ya biashara yoyote ile.
Miezi sita ya kwanza ni hatari zaidi, maana hapo biashara inaweza kufa haraka.
Katika kipindi hiki biashara ni sawa na mtoto mchanga, inahitaji kunyonya ili ikue.
Hicho ni kipindi ambacho biashara yako inahitaji zaidi kutoka kwako.
Inahitaji sana muda wako na umakini wako.
Na inahitaji sana uendelee kuwekeza fedha kwenye biashara hiyo.
Hivyo hakikisha kwenye hicho kipindi unakuwepo moja kwa moja kwenye biashara. Na hapa utaona wazi kwa nini biashara nyingi hufa pale mtu anapoanzisha akiwa mbali.
Ni sawa na kuzaa mtoto kisha kumtelekeza, hawezi kupona.
Hakikisha pia unakuwa na akiba ya mtaji katika kipindi cha uchanga wa biashara. Usitumie mtaji wote kwenye kununua bidhaa au kuandaa huduma. Hujui mambo yataendaje, hivyo kuwa na akiba ya mtaji, kadiri unavyokwenda utajifunza ambayo hukujua na unapokuwa na akiba ya mtaji unaweza kuchukua hatua sahihi.
Kipindi cha uchanga wa biashara ni kipindi ambacho biashara inakutaka ujitoe sana, ni kipindi ambacho biashara inajijenga au kufa. Weka muda, juhudi na rasilimali nyingine zinazohitajika ili biashara yako iweze kuvuka salama.
Kipindi cha pili; Ukuaji wa kasi.
Biashara huwa zinapitia vipindi vya ukuaji wa kasi. Katika vipindi hivyo biashara huwa inakuwa nzuri sana.
Wateja wanakuwa wengi na mahitaji yao yanakuwa makubwa.
Kuna wakati mpaka biashara inashindwa kuwahudumia wateja vizuri.
Hiki ni kipindi ambacho unapaswa kukua kwa kasi na biashara yako.
Wafanyabiashara wengi hukosea kwenye kipindi hiki, huridhika haraka na kudhani wameshafaulu na kujua siri ya mafanikio kwenye biashara.
Wasichojua ni huo ni msimu tu, utapita na mambo yatabadilika.
Wakati biashara yako inakwenda vizuri, jua ni kwa kipindi kifupi tu, haitadumu hivyo milele.
Hivyo kitumie kipindi hicho kwa ufanisi wa hali ya juu.
Weka juhudi kubwa kuhakikisha biashara inanufaika kweli na kipindi hiki.
Hakikisha mahitaji ya wateja yanapatikana na kazana kuwafikia wateja wengi zaidi.
Huu ni wakati pia wa kutunza akiba ya kutosha ya mtaji wa biashara, ambao utaiwezesha biashara kujiendesha pale mambo yanapobadilika.
Katika kipindi hiki cha ukuaji wa kasi wa biashara, tenga kiwango cha faida unayopata kuwa akiba ya mtaji ambao utatumika pale majira ya biashara yanapobadilika.
Katika kipindi hiki pia wekeza kwenye maeneo tofauti na biashara hiyo. Mara nyingi tunaoona biashara inafanya vizuri, tunasukumwa kuwekeza kila kitu kwenye biashara hiyo.
Lakini kumbuka uchumi hautabiriki, lolote linaweza kutokea na kuathiri sana sekta ambayo biashara yako ipo.
Utakuwa kwenye nafasi nzuri kama umewekeza kwenye sekta nyingine tofauti na sekta ilipo biashara yako kuu.
Ni muhimu biashara yako inapofanya vizuri, uanzishe biashara nyingine kwenye sekta ya tofauti.
Na pia unapaswa kuwa na uwekezaji mwingine unaokua thamani na kuzalisha faida nje ya biashara yako kuu.
Makosa ambayo wafanyabiashara wengi hufanya kwenye kipindi cha ukuaji wa kasi ni kuwa na matumizi makubwa kwenye biashara na kwao binafsi. Matumizi hayo yanameza faida yote na kuiacha biashara pabaya pale mambo yanapobadilika.
Kipindi cha ukuaji wa kasi wa biashara ni kipindi cha kuikuza zaidi biashara, kuweka akiba ya mtaji na kufanya uwekezaji nje ya biashara hiyo.

Kipindi cha tatu; Changamoto kubwa.
Kila biashara huwa inapitia kipindi cha changamoto kubwa, changamoto zinazokuwa hatari kwa uhai wa biashara.
Changamoto hizo zinaweza kuwa chanzo chake ni ndani ya biashara au nje ya biashara.
Katika kipindi hiki, biashara inakuwa ngumu sana na hatari ya kufa kuwa inaonekana wazi.
Hata juhudi ambazo zinawekwa kwenye hicho kipindi hazionekani kuleta matokeo ya tofauti.
Hiki ni kipindi cha kujifunga mkanda, kipindi cha vita. Lengo kuu la kipindi hiki ni kuivusha biashara ikiwa hai (survival).
Kwa kuwa kipindi hicho hakidumu milele, biashara inayovuka kipindi hicho ikiwa hai ndiyo inayoweza kuendelea.
Ile inayokufa kwenye kipindi hicho ndiyo inakuwa imepotea kabisa.
Hiki ni kipindi cha kupunguza mno gharama kwenye biashara, kuhangaika na yale muhimu na ya msingi pekee.
Hiki ni kipindi cha kutumia akiba uliyoweka wakati biashara inakwenda vizuri.
Unapokuwa unapitia kipindi hiki kibiashara, lengo kuu ni kuivusha biashara iliwa hai, mengine yote yanaweza kusubiri.
Hivyo jiulize na kujipa majibu kwenye hilo, naivushaje biashara kwenye kipindi hiki?
Kama ambavyo miti hupukutisha majani kipindi cha kiangazi kikali na wanyama kujichimbia ardhini wakati wa baridi kali, lazima biashara iwe na njia ya kuvuka nyakati ngumu ili isife.
Kadiri biashara inavyoweza kuvumilia nyakati za changamoto kwa muda mrefu, ndivyo inavyoweza kubaki hai na kupata mafanikio makubwa.
Maana wakati wa changamoto biashara nyingi hufa, hivyo zinazovuka salama zinakuwa na soko zuri.
Kipindi cha nne; Mabadiliko makubwa.
Biashara inapokwenda vizuri, wengi hujisahau na kuona wameshamaliza kila kitu.
Wanachosahau ni hakuna kizuri kinachodumu milele, kama ilivyo kwa magumu pia, hayadumu milele.
Biashara huwa zinafika kipindi ambacho zinahitaji kufanyiwa mabadiliko makubwa ili ziweze kuendelea.
Hapo ni pale mabadiliko ya nje yanapoilazimisha biashara ibadilike la sivyo inakufa.
Kujua kipindi hicho mapema lazima uwe mfuatiliaji wa karibu wa biashara yako. Lazima ujue kila kinachoendelea kwenye biashara.
Kwa kujua hivyo, utaona haraka pale kunapokuwa na mabadiliko.
Kipindi cha mabadiliko makubwa huwa kinataka ubadili kabisa mfumo wa biashara yako ili iweze kuendana na mabadiliko kwenye soko.
Pia kuna wakati mabadiliko makubwa yanakutaka ubadili kabisa biashara.
Mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanaleta vitu vipya, kitu kinachoua biashara nyingi za zamani.
Ni muhimu ujue mabadiliko yanayoendelea kwenye sekta ambayo biashara yako ipo ili uweze kuchukua hatua mapema.
Usiendelee kung’ang’ana na kitu ambacho hakina tena fursa ya ukuaji zaidi. Fanya mabadiliko kadiri soko la biashara yako linavyobadilika.
Na hapo hakikisha unalijua soko lako vizuri.

Rafiki, hivyo ndivyo vipindi vinne muhimu ambavyo kila biashara huwa inapitia. Vinaweza visitokee kwa mpangilio huo na wakati mwingine vinaweza kutokea kwa pamoja.
Muhimu ni uifuatilie biashara yako kwa karibu na ujue ni kipindi gani inapitia ili kuchukua hatua ambazo ni sahihi.
Tunaishi kwenye zama ambazo mabadiliko yanatokea kwa kasi kubwa, kufanya biashara kwa mazoea ni kuamua kupoteza nguvu, muda na fedha zako.
Unapochagua kuingia kwenye biashara, chagua kupambana kweli mpaka ufanikiwe na matika kipindi chochote kile usijione umeshamaliza kila kitu.
Mambo hubadilika haraka sana, usipokuwa makini utajikuta kwenye anguko kubwa.
Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani
www.somavitabu.co.tz
Ahsante, Muuza Matumaini Kocha, kwa kuendelea kutuelimisha.
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike
Ahsante sana.
LikeLike