2398; Usibadili Maamuzi, Badili Mikakati…

Umeamua kwamba ni sahihi kwako kuingia kwenye biashara.
Ni kitu ambacho umeona kinatoka ndani yako kweli.
Umeiona fursa nzuri,
Na unaona ndiyo njia ya uhakika ya kuishi kusudi lako na kuzifikia ndoto zako kubwa.

Unaingia kwenye biashara ukiwa na hamasa kubwa.
Unaona jinsi unakwenda kufanya makubwa.
Lakini kabla hujakomaa kwenye biashara, unapigwa mweleka mkubwa na kuanguka vibaya.
Unapata hasara au unakosa kabisa wateja.

Unachokimbilia kufanya ni kubadili maamuzi yako, kwa kuona hayakuwa sahihi.
Kumbuka wakati unaanza ulijiaminisha ndiyo maamuzi sahihi kabisa kufanya.
Sasa baada ya matokeo unabadilika na kuona hayakuwa maamuzi sahihi.

Huko ni kuyumba kimaamuzi na ndiyo chanzo cha wengi kuhangaika na mengi yasiyo na tija.
Watu wanafanya maamuzi mapya kila wakati, kujaribu vitu vipya kila mara na kutokupiga hatua kubwa.

Unapofanya maamuzi na ukajiaminisha ni sahihi, usikimbilie kuyabadili kwa sababu hujapata matokeo uliyotegemea. Badala yake angalia mikakati uliyotumia na iboreshe zaidi.

Mara nyingi tatizo siyo maamuzi, bali mbinu unazotumia.
Usikimbilie kubadili maamuzi yako kabla kwanza hujatumia mbinu mbalimbali na mbadala.

Ukishaamua, simamia maamuzi yako na yapambanie na siyo kukimbilia kuyabadili kutokana na matokeo unayopata.

Kutokupata matokeo unayotegemea hakumaanishi matokeo yako hayakuwa sahihi. Usiunganishe matokeo na maamuzi moja kwa moja.

Angalia mchakato unaofanyia kazi, angalia mbinu ambazo umetumia. Kuna mahali utaona hapajafanyiwa kazi vizuri.

Kocha.