Rafiki yangu mpendwa,
Vilio, sababu na visingizio vya kila mtu kwenye zama hizi ni muda.
Muulize mtu kwa nini hasomi vitabu na atakujibu hana muda.
Muulize kwa nini haanzishi au kukuza zaidi biashara yake atakuambia muda.
Muulize kwa nini haendelezi vipaji na uwezo ulio ndani yake, atalalamikia muda.

Kabla hujaendelea kusoma, hebu kwanza jibu swali hili;
Kama ungepata saa moja ya ziada kwenye siku yako, ungeitumia kufanya nini?

Kaa chini na andika majibu yako kwenye hilo swali.
Tafadhali sana usiendelee kusoma mpaka kwanza umeandika majibu hayo.
Rudi kwenye swali hapo juu, andika majibu.

Tayari, vizuri. Yatunze majibu hayo kwa sababu utayatumia hapo juu.

Vikwazo vya mafanikio vimegawanyika kwenye makundi mawili.

Kundi la kwanza ni sababu, hivi ni vikwazo vya kweli kabisa ambavyo vinamzuia kila mtu.
Sababu ni jinsi hali fulani zilivyo na zipo nje kabisa ya uwezo wako, huna namna ya kuziathiri.
Sababu zinamzuia kila mtu.

Kundi la pili ni visingizio, hivi ni vikwazo ambavyo siyo vya kweli kwa sababu havimzuii kila mtu.
Visingizio ni kitu ambacho mtu mmoja anakitumia kama kikwazo, wakati wengine wameweza kukivuka na kufanikiwa.
Kama kuna walioweza kuvuka kikwazo fulani, basi hicho siyo sababu, bali ni kisingizio tu.

Muda uko kwenye kundi la visingizio. Japo wengi wanatumia muda kama sababu, hauwezi kuwa sababu kwa kuwa kuna waliovuka.

Watu wote duniani tuna masaa 24 kwa siku, hakuna hata mmoja mwenye sekunde ya ziada, hata tajiri namba moja wa dunia, ana muda kama wako.
Walioweza kufanya makubwa wametumia muda huo huo wa masaa 24 ambao wengi walioshindwa wanaulalamikia hautoshi.

Leo nakwenda kukusaidia uondoke kwenye upande huo wa malalamiko, uachane kabisa na kisingizio hicho cha muda.
Ahadi yangu kwako ni hii, ukifanya zoezi ninalokushirikisha hapa, utapata saa moja ya ziada ambayo unaweza kuitumia kufanya yale muhimu zaidi.
Na kwa kuwa umeshajibu nini utafanya kwa saa moja ya ziada utakayokuwa nayo, utaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.

Zoezi la kufanya.
Zoezi ninalokushauri ufanye ili upate saa moja ya ziada kila siku ni hili; kila siku amka mapema zaidi ya ulivyozoea.
Kama umezoea kuamka saa 12 amka saa 11.
Kama umezoea kuamka saa 11 amka saa 10.
Na kama umezoea kuamka saa 10 amka saa 9.

Muda wowote ambao umezoea kuamka sasa, rudisha saa moja nyuma na amka mapema zaidi.
Hii ni njia ya uhakika kabisa ya kupata saa moja ya ziada kwenye maisha yako.

Na uzuri ni muda ambao huwezi kusumbuliwa na wengine, kwa sababu wengi wanakuwa bado wamelala.
Unapata muda tulivu wa kuweza kufanya makubwa na ya muhimu kwako kabla kelele za dunia hazijaanza.

Hii siyo mbinu mpya, ni mbinu ambayo imekuwepo miaka na miaka. Na miaka mingi iliyopita Benjamin Franklin amewahi kusema; kuwahi kulala na kuwahi kuamka kunamfanya mtu kuwa na afya, hekima na utajiri.

Hebu fikiria vizuri hapo rafiki yangu, kitendo cha wewe kuamka mapema kwa saa moja tu kila siku, kinakutosha kuwa na afya bora (unapata muda wa kufanya mazoezi), kuwa na hekima zaidi (unapata muda wa kusoma vitabu) na unapata utajiri pia (unawahi kuanza shughuli zako kabla ya wengine.

Mahali pengine Franklin anasema ukichelewa kuamka, inabidi ufanye kazi mara mbili ili kuwafikia wanaowahi kuamka.
Hakika kuwahi kuamka kuna manufaa makubwa mno.

Rudi kwenye majibu ya swali nililokuuliza pale juu, umeshapata saa yako moja, sasa itumie kwa umakini.
Tumia kipaumbele cha Afya, Hekina na Utajiri kupanga yake utakayofanya kwenye muda wako.
Kwa hii saa moja uliyoipata, usiitumie kwa chochote nje ya hayo matatu.
Kwa kufanya hivyo utaweza kuyaona mabadiliko ya kweli kwenye maisha yako.

Mambo ya kuzingatia ili zoezi hili liwe na mafanikio.

1. Panga kabisa utafanya nini unapoamka ili ukiamka unaenda moja kwa moja kwenye utekelezaji. Usipopanga mapema, ukiamka utapoteza muda mwingi kufikiria nini ufanye. Tayari kipaumbele unacho, kitumie.

2. Weka alamu ya kukuamsha muda huo wa mapema na iwe mbali na kitanda chako. Hakikisha ili kuizima, lazima uamke kitandani.

3. Sheria ni moja, alamu ikishalia na ukatoka kitandani, hakuna kurudi tena. Usijiambie unapumzika kwa dakika tano tu, hakuna kitu kama hicho, utakuja kushtuka nusu saa baadaye. Ukishaamka umeamka.

4. Lala mapema ili uweze kuamka naoena. Kama ukiamka mapema bado unakuwa na uchovu, lala mapema na siyo kuacha kuamka mapema.

5. Jijengee uwajibikaji utakaokulazimisha uamke mapema. Kuwa na mtu anayekusimamia kwa karibu kwenye hilo, ambaye hatakuachia kirahisi.

6. Usitumie muda wa mapema kuhangaika na mambo yasiyo na tija. Usifuatilie habari, usiingie mitandaoni. Vipaumbele vyako ni vitatu tu; #AfyaUtajiriHekima

7. Kuwa mvumilivu, siku za kwanza zitakuwa ngumu lakini kadiri unavyokwenda, tabia inajengeka na kinakuwa kitu cha kawaida kwako.

8. Usijiambie wewe siyo mzuri kwenye kuamka asubuhi, kwamba wewe ni bundi ambaye uko vizuri kwenye kukesha. Kama ukiambiea ukiamka mapema kila siku unapewa milioni moja, hutaanza kusema kwamba wewe siyo mtu wa asubuhi, utaamka mapema.  Kipaumbele cha #AfyaUtajiriHekima kinaweza kukupatia milioni moja kila siku, kwa nini usianze kuamka sasa?

9. Lala kwenye eneo tulivu ili usingizi wako uwe bora na upate pumziko la kutosha.

10. Soma kitabu cha PATA MASAA  MAWILI YA ZIADA KILA SIKU, hicho kinakupa mbinu za juu zaidi za kupata muda zaidi kwenye siku yako na kufanya makubwa. Kupata kitabu hiki, wasiliana na 0717 396 253.

Rafiki, tayari unajua nini cha kufanya, kujua ni asilimia 1, asilimia 99 iko kwenye kuchukua hatua ili maisha yako yaweze kubadilika.
Chukua hatua sasa, hiyo ndiyo namna pekee ya kunufaika na haya mazuri unayoyajua.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
www.somavitabu.co.tz