2399; Jenga nguvu ya ushindani…
Kama kuna vitu viwili vinavyofanana na ambavyo vipo sehemu moja, kimoja hakina umuhimu.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara. Kama kuna biashara mbili zinazofanana kwa kila kitu, moja siyo muhimu.
Na kama biashara zinazofanana ni nyingi, nyingi pia zinakuwa siyo muhimu.
Inakwenda hata kwenye kazi. Kama kuna wafanyakazi wawili wanafanya kazi moja na wanafanya kwa namna inayofanana, mmoja hana umuhimu.
Kitu kikubwa cha kujifunza hapa ni kwamba kama huna kinachokutofautisha na wengine, basi huna umuhimu.
Huna nguvu ya ushindani na yeyote anaweza kukuangusha.
Nguvu ya ushindani inajengwa kwa kujitofautisha, kwa kufanya kile ambacho unaowalenga hawawezi kukipata mahali pengine isipokuwa kwako.
Kama huna kinachokutofautisha na wengine, maana yake umeamua kwamba wewe siyo muhimu na hakuna sababu ya watu kuwaacha wengine na kuja kwako.
Usikubali kujiangusha wewe mwenyewe, tengeneza kitu kinachokutofautisha wewe na wengine kwenye kila unachofanya.
Kocha.