Mtandao wa intaneti umefungua fursa nyingi za watu kuweza kuingiza kipato kwa njia mbalimbali.

Moja ya njia hizo ni kuuza bidhaa na huduma mbalimbali kwa watu walio popote duniani.

Unaweza kuuza kitu chako kwa mtu aliye nchi yoyote ile duniani.
Lakini changamoto kubwa kwa sasa ni njia ya kuweza kulipwa.

Kama unauza vitu mtandaoni ukiwa Tanzania na mtu akanunua akiwa nje ya ncho, hasa Ulaya na Amerika, ni vigumu sana kupokea malipo moja kwa moja.

Hapa tutakwenda kushirikishana hatua za kuchukua kwenye hili.
Kabla ya kuziona hatua hizo, tusome maoni ya msonaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.

“Nashukuru Sana brother makirita Amani. Mimi changamoto yangu nataka kuanza biashara ya Affiliate market kupitia blog kwa mfano nijiunge na makampuni makubwa Kama Amazon niuze bidhaa za kampuni nyingine humo katika Amazon na pia wao niwauzie za kwao na wanilipe commission. Sasa changamoto yangu ni jinsi ya kulipia huduma na jinsi ya kulipwa kutoka nchi za marekani na ulaya. Kwa kifupi naomba ufafanuzi wa ile getway Kama njia za kulipia huduma na kulipwa Asante Sana.” – Saidi K. T.

Mpaka sasa hatujawa na mfumo wa malipo wa kuweza kupokea fedha moja kwa moja kutoka nje ya bara la Afrika.

Njia maarufu ambazo zimekuwa zinatumika kama Paypal, Stripe na Visa unaweza kuzitumia kutuma fedha pekee, lakini kupokea huwezi.
Hii ni kutokana na sera za kifedha zilizopo sasa.

Kumekuwa na mapendekezo mengi kwenye marekebisho ya hili, na huenda likafanyiwa kazi na milango ya malipo ikafunguliwa.

Lakini kwa kipindi hiki ambapo bado milango ya kulipwa moja kwa moja haijafunguliwa, unaweza kutumia njia zifuatazo.

1. Kutumiwa fedha moja kwa moja.
Kupitia huduma kama Western Union na Money Gram unaweza kutumiwa fedha moja kwa moja.
Kwa njia hiyo mtu unayemuuzia bidhaa au huduma anakutumia fedha na wewe kwenda kuzitoa.
Njia hiyo ni rahisi, ila kwa nchi zilizoendelea hawaiamini sana, hivyo siyo wote watakaokuwa tayari kuitumia.
Ila kama unauza kitu cha kipekee ambacho wateja wanakipata kwako tu, watakuwa tayari kutumia njia hiyo.

2. Kutumia fedha unazolipwa kununua vitu mbalimbali.
Unaweza kuwa na akaunti ambayo unalipwa fedha kutoka nje mfano Paypal. Kwa kuwa changamoto ni kuzitoa, unachofanya ni kutumia fedha hizo kulipia vitu mbalimbali mtandaoni.
Kama kuna vitu unanunua kutoka nje, badala ya kutuma fedha, unalipa kwa kutumia ulizolipwa.
Kwa hiyo unaweza kuuza vitu, ukalipwa, ukatumia malipo hayo kununua vitu vingina unavyohitaji au unavyoweza kuja kuuza hapa nchini na ukalipwa moja kwa moja.

3. Teka soko la Afrika.
Kulipwa kwa nchi za Afrika ni rahisi zaidi kwa sababu kuna njia mbadala za malipo kama mitandao ya simu.
Hivyo unaweza kuelekeza nguvu zako kuuza kwa soko la Afrika ambapo wateja wanaweza kukulipa kwa njia za mitandao ya simu au Western union ambayo tayari imezoeleka.

Njia hizi ni nzuri kwa bidhaa au huduma ambazo unauza mwenyewe moja kwa moja. Lakini kama unataka kuuza kama wakala hasa wa makampuni makubwa kama Amazon, kulipwa ni vigumu kwa hali tuliyonayo sasa.
Labda kama utatumia njia ya kununua vitu kwa malipo yako.

Ndiyo maana nimekuwa nashauri sana wanaoanzisha blog, walenge kutengeneza hadhira ambayo wataiuzia bidhaa na huduma moja kwa moja badala ya kutegemea njia ya uwakala au matangazo.

Kwenye kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA KIPATO KWA KUTUMIA BLOG, ambacho nashauri kila mtu akisome, nimeeleza jinsi ya kutengeneza hadhira inayokuamini na kisha kuitumia kuingiza kipato mtandaoni.
Kukipata kitabu hiki, wasiliana na namba 0717 396 253.

Usikubali kuwa tu mtumiaji wa mtandao wa intaneti, kuwa pia mtu unayeingiza kipato kwenye mtandao huo. Chukua hatua sasa kwa kusoma kitabu cha JINSI KUTENGENEZA KIPATO KWA KUTUMIA BLOG na uanze kunufaika.

Kama una changamoto inayokuwa kikwazo kwa mafanikio yako, unaweza kupata ushauri kwa kujaza fomu hii; http://bit.ly/ushauri

Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz