2403; Itumie hiyo nguvu isikuumize…

Kipindi cha nyuma kidogo huko Moshi kilianzishwa kiwanda cha pombe iliyoitwa Banana.

Ni pombe kali iliyotengenezwa na ndizi. Ilikuwa mwenye duka anapoenda kununua, mpaka anafikisha dukani, kwenye kreti chumba mbili mpaka tatu zinapasuka zenyewe.

Wakati wa kufungua pombe hiyo ilipaswa kufanywa taratibu la sivyo ilimwagika yote na mtu kukosa kitu cha kunywa.

Yote hayo yalitokana na ukali wa pombe hiyo ambao ulikuwa na nguvu ya kupasua chupa au kumwagika yote pale inapofunguliwa kwa haraka.

Ndani yetu huwa tunapata nguvu ya aina hiyo, nguvu ambayo tusipoitumia vizuri inapelekea uharibifu.

Pata picha unapokuwa umepatwa na hasira kali, unakua na nguvu kubwa ambayo inakusukuma ufanye kitu. Ukikosa udhibiti unajikuta umepiga mtu na kumuumiza au kuharibu vitu.

Unapaswa kujua kila nguvu iliyo ndani yako na kuitumia kufanya mambo yenye tija. Kwani usipotumia nguvu kwa namna hiyo, itakupelekea kufanya uharibufi, kwako mwenyewe, kwa wengine au kwa vitu mbalimbali.

Hasira, chuki, vinyongo na msongo ni nguvu kubwa zinayokuwa zimejikusanya ndani yako ambazo kama huna njia ya kuzitawanya zitaleta uharibifu.

Tamaa na wivu ni nguvu nyingine za kuwa nazo makini.
Katika wakati wowote, kuwa na njia za kutumia nguvu hizo za ndani yako, ili zisijikusanye na kuleta uharibifu.

Kanuni ya fizikia inasema nguvu haiwezi kutengenezwa wala kuharibiwa, ila inaweza kubadilishwa kutoka mfumo mmoja kwenda mwingine.

Hiyo ina maana kwamba kama una hasira ndani yako, hiyo nguvu ya hasira haitaisha yenyewe. Landa utaitumia lwa uharibifu au kwa namna njema.

Ndiyo maana kila wakati unapaswa kuwa na kitu chenye manufaa cha kufanya ambacho unapeleka nguvu inayojikusanya ndani yako.

Unaweza kupeleka nguvu hiyo kwenye kufanya kazi zako au kufanya mazoezi.
Hakikisha hakuna nguvu inabaki tupu ndani yako na kukupeleka kwenye uharibifu.

Tumia kila nguvu kwa matumizi mema ili uweze kufanya makubwa.

Uzuri ni kwamba nguvu inapokuwa inajikusanya ndani yako unaisikia kabisa, hivyo ni wewe kuipeleka kwenye matumizi mazuri kabla haijakupeleka kwenye uharibifu.

Ukiujua mwili wako mwenyewe, utaweza kuutumia vizuri kwa mafanikio yako.

Kocha.