Rafiki yangu mpendwa,

Rafiki yetu Eng Enelisa Andengulile ameandika kitabu cha historia ya maisha yake ambacho amekipa jina; NGUVU YA IMANI, Safari Ya Maisha Yangu.

Ni kitabu ambacho ameeleza kwa kina yale aliyopitia kwenye maisha yake mpaka pale alipofika sasa.

Na kama jina la kitabu lilivyo, ni kweli Enelisa ameweza kufika pale alipo kwa nguvu ya imani. Pamoja na kupitia magumu ambayo yangeweza kumkatisha tamaa, yeye hakukubali, aliendelea kupambana na mpenyo ukapatikana.

Hiki ni kitabu ambacho nashauri kila mwenye kiu ya mafanikio akisome, kwani kitakuonyesha hata kama unapitia ugumu wa aina gani, ni marufuku kukata tamaa. Maana unapovumilia kwa muda mrefu, fursa nzuri huwa zinakuja.

Kutakuwa na uzinduzi mdogo wa kitabu hiki ambao utafanyika Morogoro siku ya jumapili tarehe 01/08/2021.

Kushiriki uzinduzi huu au kupata kitabu popote ulipo Tanzania, wasiliana na namba; 0755 503 514.

Rafiki, kama nilivyokueleza hapo juu, hiki siyo kitabu cha wewe kukosa. Kama umekuwa unasoma kazi zangu, basi kitabu hiki ni sehemu muhimu kwako kupata ushuhuda na hamasa ya kuendelea na mapambano.

Eng Enelisa alinipa upendeleo wa kuandika dibaji ya kitabu hiki cha NGUVU YA IMANI, na hapo chini ni dibaji niliyoandika. Isome na wasiliana na 0755 503 514 ujipatie nakala yako ya kitabu.

DIBAJI

Kila mtu ni kitabu kinachotembea, hii ni kauli ambayo nimekuwa nawapa watu kwenye ushauri na mafunzo mbalimbali ninayatoa.

Nimshukuru sana Mhandisi Enelisa Andengulile kwa kusikiliza kauli hiyo na kuifanyia kazi, kwani tumepata fursa ya kujifunza mengi kupitia maisha yake.

Kila mtu kuna mengi aliyopitia kwenye maisha yake, tangu anazaliwa, anakua, anasoma na kufanya kazi au biashara mbalimbali. Mambo hayo yana funzo kubwa kwa mtu mwenyewe na kwa watu wengine pia.

Tatizo kubwa la jamii zetu ni huwa hatuweki uzoefu huo wa maisha kwenye maandishi kwa namna ambayo wengine wanaweza kunufaika na hilo. Nimekuwa nashauri sana tuvunje utamaduni huo, tujenge utamaduni wa kuandika uzoefu wetu kwani una msaada kwa wengi.

Nimekuwa nashauri kila mtu aandike kitabu kuhusu maisha yake, hata kama hakitasomwa na dunia, basi kitasomwa na vizazi vyake, yaani watoto, wajukuu, vitukuu na vizazi vingine vinavyoendelea.

Wengi wetu tumeanzia maisha katika hatua sifuri, yaani hatukupewa mwongozo wowote na wazazi au walezi wetu, zaidi ya yale malezi ya kawaida. Lakini wazazi wetu hao walipitia mambo mbalimbali kwenye maisha, ambayo yaliwapa mafunzo makubwa, ila hatujaweza kunufaika na mafunzo hayo waliyopata.

Unaweza kuwa mtoto na kila siku unakula chakula nyumbani, lakini hujui ni magumu kiasi gani wazazi wako wamepitia mpaka ukapata chakula hicho. Kumbe kuna siku hakuwa na fedha kabisa, akapambana kwa kila namna mpate chakula. Wewe unakua ukijua maisha yanaenda sawa siku zote, siku unapokuja kukutana na changamoto kama ambayo wazazi wako walipitia, unajikuta njia panda, hujui ufanye nini.

Lakini kama mzazi wako angekuwa ameandika kitabu kwa yale aliyopitia kwenye maisha, angekuwa amekupa uzoefu wake na huo ungekusaidia sana.

Hivyo kwa sisi wazazi wote wa kizazi cha sasa, ni jukumu letu kuhakikisha watoto wetu hawaanzii hatua sifuri kwenye maisha yao. Tuhakikishe uzoefu tulioupitia kwenye maisha, uwe mzuri au mbaya tunauweka kwenye maandishi, kitu ambacho kitadumu miaka na miaka. Kila unalopitia kwenye maisha yako, linakuja na funzo fulani, ni ubinafsi kutaka kubaki na funzo hilo wewe mwenyewe.

Kwa haya machache, nikushauri sana ndugu msomaji wa kitabu hiki cha historia ya maisha ya Mhandisi Enelisa Andengulile, kikawe chachu ya wewe kukaa na kuandika kitabu cha historia ya maisha yako pia.

Chukua huu kama wajibu wako wa kuhakikisha vizazi vyako havianzii sifuri kama ulivyoanza wewe. Kwa yale yote uliyopitia kwenye maisha, iwe ni kufanikiwa au kushindwa, weka kwenye maandishi, ni hazina kubwa kwa vizazi vyako.

Katika huduma ninayotoa ya Ukocha wa mafanikio, nimebahatika kufanya kazi na watu wengi, ambapo nakuwa mwalimu na mshauri wao wa karibu na kushirikiana kwenye yale wanayofanya ili kupiga hatua na kufanikiwa. Nikiri wazi kwamba Enelisa amekuwa mwanafunzi wa tofauti kabisa na sikuwa najua kwa nini mpaka niliposoma kitabu chake hiki. Licha ya kuwa na umri mkubwa kuliko mimi na kuweza kuwa hata mama yangu, amekuwa msikivu, mtu aliye tayari kujifunza na kuchukua hatua na pale ninapomwambia hapo unakosea au siyo sawa, amekuwa akijifunza na kuchukua hatua sahihi.

Kwa uzoefu wangu wa kufanya huduma hii ya ukocha, kuna makundi ya watu ambayo huwa ni wagumu sana kusikiliza ushauri sahihi wa kimafanikio.

Mhandisi Enelisa yuko kwenye makundi mawili ambayo ni wasomi na watu ambao umri wao umekwenda (zaidi ya miaka 50). Watu hawa huamini tayari wanajua kila kitu hivyo hawana kipya cha kujifunza. Ni imani yao hiyo isiyo sahihi ndiyo imekuwa inawafanya wengi wanaanguka kwenye mengi wanayofanya. Lakini Enelisa ni tofauti kabisa, ni mtu ambaye yuko tayari kujifunza na kuchukua hatua na anaposhauriwa anazingatia na kufanya kwa ubora zaidi.

Kuna mambo mengi mno ya kujifunza kupitia kitabu hiki. Wakati Mhandisi Enelisa amenipa nafasi ya kusoma kitabu hiki na kuandika dibaji hii, mimi binafsi nimeorodhesha mambo 20 ambayo nimejifunza kupitia maisha yake, ambayo nitayatumia kwenye maisha yangu na kuwashauri wengine kupitia huduma ya ukocha ninayotoa.

Kwa kuwa umeshakipata kitabu hiki, naamini unakwenda kujifunza mengi mno, ambayo kama utayafanyia kazi basi utapiga hatua kubwa kwenye maisha yako. Nitaomba nikushirikishe matano makubwa niliyojifunza, halafu wewe mwenyewe utaendelea kujifunza mengi kutoka kwenye kitabu hiki kizuri.

Jambo la kwanza kubwa nililojifunza kupitia maisha ya Mhandisi Enelisa ni nguvu ya imani isiyoyumbishwa na chochote.

Ametushirikisha mapambano aliyopitia wakati anasimama kwenye wokovu, kwa kweli ni mapambano yaliyokuwa makubwa na mazito kwake. Lakini kwa kusimama kwenye imani, Enelisa ameweza kushinda na mpaka leo, miaka zaidi ya 30 baadaye, bado amesimama imara kwenye imani.

Na hapa ndipo nimejifunza kwa nini Enelisa amekuwa mwanafunzi wa kipekee kwenye huduma yangu ya ukocha, ni kwa sababu ana imani isiyotetereshwa na chochote. Imani hii ina nguvu kubwa mno ya kumfikisha kwenye mafanikio makubwa.

Wakati nasoma aliyopitia wakati akipambana kusimamia imani yake, kuna wakati mpaka mwili ulinisisimka. Kupata picha ya mtoto, tena binti kusimamia imani ambayo familia na hata ukoo mzima uliipinga siyo kitu rahisi. Kama asingekuwa na msimamo asingeweza kushinda vita ile na huenda tusingemjua leo, maana maisha yake yasingekuwa haya aliyoweza kufikia.

Jambo la pili ni nguvu ya kutenda miujiza ambayo iko ndani ya kila mmoja wetu. Maisha ya Enelisa, tangu kuzaliwa kwake mpaka alipofika sasa ni mfululizo wa miujiza.

Anaeleza kwamba hata wazazi wake walimwambia hawakutaka azaliwe, walitaka sana kupata mtoto wa kiume ila akaja wa kike. Hivyo waliona hana manufaa makubwa kwao.

Lakini maisha yake yamefanyika baraka kubwa kwa wazazi, ndugu wengine na jamii kwa ujumla. Maisha yake ya shuleni, tangu shule ya sekondari, kufaulu kwenda chuo cha ufundi na kwenda chuoni huku akiwa hajui maisha yataendaje ni miujiza mitupu.

Kumaliza masomo ya chuo, kupata kazi, kuchumbiwa na kuolewa, kukosa kazi na kupambana na maisha magumu ya mtaani bila ya ajira ni miujiza mingine tunayoiona ikitendekea kwenye maisha yake.

Kama nilivyoeleza kwenye kitabu nilichoandika kinachoitwa UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA, Enelisa amedhihirisha hilo wazi. Kwa magumu ambayo amepitia, kwa mtu mwingine ingekuwa rahisi sana kukata tamaa na kusema huwezi au haiwezekani. Lakini kwa imani imara aliyokuwa nayo Enelisa, aliweza kukaribisha miujiza mbalimbali kwenye maisha yake.

Ninachotaka kukuambia hapa ndugu msomaji ni kimoja, haijalishi unapitia nini, kuna miujiza mikubwa inayoweza kutendekea kwenye maisha yako. Kama huamini soma namna Enelisa alipata ada wakati ambapo hakuwa na tumaini lolote, pia soma jinsi alivyoweza kupambania uhai wa mtoto wake aitwaye Emanuel na akavuka salama.

Jambo la tatu ni nguvu ya matendo. Katika malezi huwa tunahangaika sana kuwaeleza watoto nini wanapaswa kufanya, lakini ambacho hatuelewi vizuri ni kwamba watoto hao huwa hawatusikilizi, ila wanatuangalia.Unaweza kuwaambia watoto maneno mengi uwezavyo, lakini watakachojifunza kwako ni yale unayofanya kwenye maisha.

Enelisa ametushirikisha jinsi ambavyo alijifunza utulivu wa maisha ya ndoa kupitia wazazi wake. Anaeleza jinsi ambavyo katika kipindi chote cha maisha yake, hakuwahi kuwaona wazazi wake wakigombana au kupigana. Hilo lilimpa udadisi na kumuuliza mama yake, ambaye alimjibu huwa wanatofautiana na baba yake, lakini wanajua jinsi ya kutatua tofauti zao. Hapo Enelisa alitoka na funzo kubwa, ambalo ameliishi kwenye maisha yake pia.

Tunajifunza kitu kikubwa sana hapa kwenye malezi, tunaweza kulalamika kwa nini watoto hawatusikilizi, lakini wanatuangalia sana. Chochote tunachotaka kijengeke kwa watoto wetu, lazima sisi tukiishi kama mfano kwao.

Huwezi kumwambia mtoto ulevi ni mbaya huku wewe unalewa kila siku. Huwezi kumwambia mtoto anapaswa kumheshimu mwenza wake kwenye ndoa huku nyie wazazi mnagombana na kurushiana maneno makali mbele yao. Watoto wanaangalia kuliko kusikiliza hivyo tuwe makini na mifano tunayowaonesha.

Jambo la nne ni uvumilivu na ung’ang’anizi. Nikiri wazi nilidhani ninamfahamu Enelisa kwa kipindi chote ambacho amekuwa kwenye huduma yangu ya Ukocha, lakini baada ya kusoma kitabu hiki, nikagundua nilikuwa sijamfahamu vizuri.

Naweza kusema Enelisa ni mmoja wa watu wenye uvumilivu na ung’ang’anizi mkubwa mno kuwahi kuwafahamu. Kama asingekuwa na ung’ang’anizi huu, ndoto zake nyingi zisingefikiwa.

Tangu akiwa shule alipenda sana kuwa mhandisi wa umeme. Kwa mfumo wetu wa elimu kila mtu anaijua njia rahisi ni kusoma kidato cha kwanza mpaka cha sita kisha kwenda chuo kikuu kusomea uhandisi. Lakini safari ya Enelisa haikuwa hivyo, kwanza hakufaulu darasa la saba, hivyo akarudia tena mwaka mzima. Alipomaliza kidato cha nne akachaguliwa kwenda chuo cha ufundi kusomea ngazi ya cheti kwenye uhandisi wa umeme. Huko nako alilazimika kurudia mwaka mmoja.

Akasoma chuo cha ualimu wa ufundi na hatimaye ndiyo akaja kusoma chuo kikuu fani ya uhandisi wa umeme. Hapo umri umekwenda na ana majukumu ya kifamilia. Lakini aling’ang’ana kuhakikisha anafikia ndoto yake. Hata wakati ambapo hakuwa na kazi, alipambana kwa kila namna na maisha yakaenda.

Na sasa anapambana kukamilisha ndoto nyingine ambayo amekuwa nayo pamoja na mume wake ya kuwa na taasisi ya kutoa mafunzo. Wamekuwa na wazo hilo mara kwa mara na kuchukua hatua za kuanzisha vituo vya mafunzo ya ziada (tuition) lakini sasa ndiyo wameamua kupambana hasa kukamilisha ndoto ya kuwa na chuo chao cha ufundi cha Lupyana. Hapa naomba nikushirikishe siri moja ambayo huenda hutakuja kuijua, kwa sababu nina uhakika huko mbeleni chuo hiki kitakuwa kikubwa sana na watu watasema ona watu hawa walivyo na bahati ya kuwa na chuo kikubwa. Lakini ambacho hawataona ni mapambano wanayopitia sasa.

Mimi kama Kocha wake najua nini anapitia katika kukijenga chuo hiki sasa na nikueleze tu, kama siyo mtu mvumilivu na king’ang’anizi, angeshaamua kuachana nacho na kufanya mambo mengine. Lakini kwa imani isiyotetereka aliyonayo nina uhakika pasi na shaka yoyote, chuo cha ufundi cha Lupyana kitakuja kuwa chuo kikubwa na kitakachokuwa mkombozi kwa kuwapatia ujuzi bora watu wengi ili waweze kuyaendesha maisha yako.

Jambo la tano ni madhara ya kutegemea chanzo kimoja pekee cha kipato. Kupitia kitabu hiki cha Enelisa, tunajifunza wazi kabisa madhara ya kuwa na chanzo kimoja tu cha kipato, hasa kinapokuwa mshahara.

Kuna wakati kwenye maisha yake Enelisa alipata kazi ya ufundi umeme wa kwenye kiwanda cha huko Mbeya, kazi ikawa inamlipa vizuru na hapo akawa na uhakika wa maisha. Naweza kusema mshahara ule ulimlevya na kuona ameshamaliza kila kitu. Ni mpaka pale kiwanda kilipofilisika na kufungwa na kujikuta hana tena kazi na hana kipato. Hii ilipelekea yeye na mume wake wapitie maisha magumu mno, maana wote hawakuwa na kazi. Lakini hilo liliwapa funzo, kwani wakati mwingine walipokosa tena kazi, baada ya serikali kufuta mafunzo ya ufundi kwenye shule za sekondari, angalau hapo walikuwa na kilimo kilichosaidia maisha yao yasiwe magumu kama kipindi cha awali.

Hapa Enelisa anatupa funzo kubwa sana, unapokuwa na chanzo kimoja pekee cha kipato, siku chanzo hicho kinapokauka, unajikuta kwenye hali mbaya mno kimaisha. Hivyo haijalishi unafanya kazi au biashara gani na inakulipa kiasi gani, kuwa na vyanzo mbadala vya kipato. Hakuna aliyejifunza somo hili vyema kama Enelisa mwenyewe.

Kwenye huduma yangu ya ukocha huwa kuna utaratibu wa kujifanyia tathmini kila mwezi na mtu anatuma njia zote anazotumia kuingiza kipato. Katika wote walio kwenye huduma hii, Enelisa ndiye amekuwa akiorodhesha vyanzo vingi vya kipato kuliko wengine. Kuna wakati anaorodhesha vyanzo mpaka kumi. Awali sikuwa najua kwa nini, ila baada ya kusoma kitabu hiki na kujua aliyopitia, ninaelewa. Na kama kauli ya Kiswahili inavyosema, ukishaumwa na nyoka, unaogopa hata jani.

Ndugu msomaji, kama nilivyokuambia kuna mengi mno ya kujifunza kutoka kwenye kitabu hiki cha Mhandisi Enelisa Andengulile, haya matano ni machache na muhimu ila endelea kusoma kitabu hiki, utaondoka na mengi yatakayokuwa msaada mkubwa kwenye maisha yako.

Nimalize kwa kukuomba na kukusihi sana, kama bado hujaandika kitabu kinachohusu maisha yako au uzoefu ambao umeupata kwenye mambo mbalimbali uliyopitia kwenye maisha, basi anza mchakato huo sasa. Siyo tu kwa manufaa yako, bali ni kwa manufaa ya vizazi vyako pia. Kocha Dr. Makirita Amani, Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. http://www.amkamtanzania.com

Rafiki, hiyo ni dibaji niliyoandika kwenye kitabu cha NGUVU YA IMANI. Dibaji hiyo nimeshirikisha matano makubwa kati ya mengi niliyojifunza.

Pata nakala yako ya kitabu leo ili ujifunze mengi mazuri kwa safari yako ya mafanikio.

Kupata kitabu wasiliana na 0755 503 514

Kama nilivyosisitiza kwenye dibaji, kila mtu anapaswa kuandika kitabu kwenye maisha yake. Kama upo tayari karibu tufanye kazi pamoja, nikushike mkono na kukuongoza mpaka ukamilishe kitabu chako.

Unachohitaji ni kitu kimoja tu, utayari, mengine yote tutayafanyia kazi, hata kama hujii unataka kuandika kuhusu nini.

Kama upo tayari kuandika kitabu, tuwasiliane kwa namba 0717 396 253.

Rafiki yako anayekupenda sana,

Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani

http://www.somavitabu.co.tz