2404; Nyenzo Muhimu Za Kujijengea Kwenye Maisha…

Ni Mwanasayansi Archimedes aliyesema nipe mtarimbo mrefu na mahali pa kuuegemeza na nitaweza kuisogeza dunia.

Alisema hayo kwa kujua nguvu ya nyezo, ambapo nguvu kidogo inaweza kuleta matokeo makubwa mno.

Unatumia nyenzo kwenye shughuli zako za kawaida.
Kung’oa msumari kwenye mbao siyo rahisi kwa mkono pekee, ila kwa nyundo ni rahisi, kwa sababu nyundo inatumia kanuni ya nyenzo.

Kufungua chupa ya soda kwa mkono pekee siyo rahisi, ila kwa kifaa cha kufungua chupa ni rahisi kwa sababu ya nyenzo.

Kanuni hiyo ya nyenzo unaweza kuitumia kwenye maisha yako pia na ukaweza kuzalisha matokeo makubwa kwa kuweka juhudi kidogo tu.

Kuna nyenzo tano muhimu unazopaswa kujijengea kwenye maisha yako ili kufanya makubwa.

Moja ni tabia nzuri na chanya.
Huwa tunajenga tabia na kisha tabia zinatujenga. Kama kuna kitu unataka kukifanya kwenye maisha yako, kigeuze kuwa tabia.
Ikishakuwa tabia, haiwi ngumu kwako kufanya.

Mbili ni mazingira yanayokuzunguka. Tengeneza mazingira yanayorahisisha wewe kufanya unachotaka au yanayoweka ugumu kwenye kufanya usichotaka.
Kama unataka kuacha pombe lakini unakaa na marafiki zako baa, unajidanganya.

Tatu ni muda, gatua majukumu yote yanayoweza kufanywa na wengine au na teknolojia na utumie muda wako kwa yale muhimu pekee.
Muda una ukomo, huwezi kuutumia kwa kila kinachokuja mbele yako, weka vipaumbele vyako sawa na yale yasiyo muhimu achana nayo.
Pia tumia muda wa wengine kuwesa kufanya zaidi.

Nne ni fedha, tumia fedha zako kwa mambo yanayoziongeza zaidi na siyo kuzipunguza. Badala ya kutumia, wekeza ili zizalishe.
Pia tumia fedha za wengine kukamilisha yale muhimu.

Tano ni ushawishi, chagua wachache ambao kwa kuwa na ushawishi kwao itapata yale unayotaka kwa urahisi zaidi. Toa ili iweze kupata zaidi baadaye.
Pia tumia ujuzi na uzoefu wa wengine ili kupiga hatua zaidi.

Usitegemee juhudi zako pekee kufanya makubwa, utachoka haraka na kushindwa.
Tumia nyenzo mbalimbali ili kwa juhudi kidogo uweze kuzalisha matokeo makubwa.

Kocha.