Rafiki yangu mpendwa,
Kuna takwimu ambazo siyo nzuri sana lakini zimekuwepo kwa muda mrefu.
Takwimu hizo ni asilimia kubwa ya watu wanaostaafu kazi, hufariki ndani ya miaka mitano ya kustaafu kwao.

Wengi wamekuwa wanatumia sababu ya maisha kubadilika, hasa pale wanaposhindwa kuyatumia mafao yao vizuri, kitu kinachopelekea wayapoteze na kupata mshtuko mkubwa.
Ndiyo hiyo inaweza kuchangia, lakini kuna sababu nyingine kubwa zaidi ambayo watu huwa hawaiangalii.

Sababu hiyo kubwa zaidi ni kukubali kiroho kwamba kazi ya mtu hapa duniani imeshaisha na hana tena matumizi. Ukishakubali hivyo ndani yako, afya inakuwa dhoofu na kufariki inakuwa rahisi.

Mtu anapokuwa anafanya kazi, ndani ya roho yake anajua bado ana uhitaji mkubwa.
Anapokuwa ana watoto wadogo anaowalea, anajua kabisa wanamtegemea sana.
Hivyo maisha yake yanakuwa na kusudi, hata kama kusudi hilo ni kuwahi kazidi au kumkwepa bosi.

Kusudi lolote lile linakuwa limemtinga mtu na anakuwa imara kiafya ili alikamilishe.
Inapotokea mtu amestaafu na hana tena kitu kinachomsukuma kuamka asubuhi, kiroho anakata tamaa na kuona hana tena matumizi hapa duniani.
Anakosa msukumo na hilo linapelekea afya yake kuwa dhoofu na kufariki haraka.

Wachina huwa wana sikukuu yao ya kuadhimisha mwaka wao mpya. Hiyo huwa ni sikukuu inayoheshimiwa sana na kila mtu, katika kipindi hicho huwa hawafanyi kazi, badala yake wanakutana pamoja kusherekea sikukuu hiyo.

Jambo moja limekuwa linaeashangaza wengi kwamba kila baada ya sikukuu hizo za Wachina, wazee wengi huwa wanafariki dunia. Wengi walikuwa wanadhani kwamba hilo linatokana na kula kwa kupitiliza kipindi cha sikukuu.
Lakini tafiti zinaonyesha sababu ni tofauti.

Kwenye sherehe hizo za Wachina, wazee huwa wana majukumu maalumu na muhimu ambayo huwa wanayafanya. Hivyo sikukuu zinavyokaribia, kila aliye mzee sana anajua ana wajibu mkubwa mbele yake na hilo linamsukuma aendelee kuwa hai hata kama afya siyo nzuri.

Mara baada ya sikukuu kuisha, wazee hao wanajiona wamemaliza kazi yao na hapo wanakata tamaa kiroho na kufa.
Ni jambo la kushangaza lakini ndivyo lilivyo, nguvu ya kiroho ndiyo inaendesha maisha yetu, isipokuwepo chochote kinaweza kusababisha kifo.

Kwa kujua hilo, tunajifunza siri kubwa sana ya kuishi miaka mingi, kutokustaafu.

Shigeaki Hinohara alikuwa daktari wa Kijapani aliyefariki mwaka 2017 akiwa na miaka 105. Mpaka anafariki dunia, daktari huyo alikuwa bado anatibu wagonjwa wake na alikuwa na miadi ya miaka miwili mbele.
Yaani mpaka anafariki, alikuwa na miadi ya kuwaona wagonjwa kwa miaka miwili zaidi.

Kwenye moja ya mahojiano yake, alipoulizwa nini siri ya yeye kuishi miaka mingi, Shigeaki Hinohara alijibu ni kutokustaafu.
Alipoulizwa nini kinampa nguvu ya kuweza kuendelea na kazi licha ya kuwa na miaka zaidi ya 100 alijibu ni kupenda anachofanya.

Shigeaki Hinohara alieleza hana sheria nyingine nyingi zaidi ya hizo mbili na hapendi kuuchosha mwili wake na sheria nyingi kama ale nini au alale wakati gani. Yeye alichojua ni hakupaswa kustaafu na alipenda anachofanya.

Rafiki, tunapata somo kubwa sana hapa, kama tunataka kuwa na maisha bora na yenye afya imara, kiroho tunapaswa kujua kuwa bado tuna umuhimu mkubwa, hivyo hatupaswi kustaafu.

Umri wa kustaafu ambao ni miaka 60 mpaka 65 uliwekwa miaka mingi iliyopita, kipindi ambacho mtu kuvuka miaka 60 ilikuwa nadra sana.
Lakini sasa afya zimekuwa bora na watu wanaishi miaka zaidi ya 80, huku wengine wakifika 100.

Sasa hebu fikiria umestaafu kazi ukiwa na miaka 60, halafu upo tu huna cha kufanya kwa miaka 40? Huwezi kufikisha miaka hiyo.
Lakini kila siku unapoamka ukiwa na wajibu wa kufanyia kazi, unapokuwa na kusudi ndani yako, kiroho unajiona  bado ni muhimu na unapambana kuendelea kuwa hai.

Rafiki yangu, tengeneza mazingira ambayo hutastaafu kabisa kwenye maisha yako, mazingira ambayo utafanya kazi mpaka siku unakufa.

Kama umejiajiri au unafanya biashara, chagua kufanya kile unachokipenda sana, ambacho kwako siyo kazi, unaona kama mchezo tu na kifanye kila siku ya maisha yako.

Kama umeajiriwa jua kuna siku utastaafishwa kwa lazima, anza kujiandaa mapema ili unapostaafu kazi uwe na kitu cha kuendelea kufanya kila siku.
Anza biashara yako mapema wakati bado uko kwenye ajira, ili unapostaafu ni kuiendeleza tu na siyo kuanzia tena chini penye hatari kubwa.

Na kikubwa zaidi, hakikisha kila wakati wa maisha yako una mambo haya mawili;

Moja ni kulijua kusudi kubwa la maisha yako na kuliishi kila siku. Jua maisha yako ni muhimu na yana manufaa kwa wengine.
Hilo linakufanya uone bado ni muhimu kiroho na uendelee kupambana.

Mbili ni kuwa na ndoto kubwa unazozifanyia kazi. Haijalishi umefika juu kiasi gani, endelea kuwa na ndoto kubwa. Haijalishi umri wako ni mkubwa kiasi gani, endelea kuwa na ndoto kubwa.
Kila siku jikumbushe ndoto zako kubwa na pambana kuzifikia.
Hilo litakufanya uone bado una wajibu mkubwa na kuwa imara kiroho.

Siku unayoamka hujui kusudi lako na huna ndoto zinazokusukuma, ndiyo siku unaiambia asili kwamba kazi yako hapa duniani imeisha na kinachofuata ni kifo.

Kila mtu atakufa, lakini wengi wanakufa kabla ya muda wao kwa sababu wanakubali kustaafu kazi zao.
Wewe kataa hili, pambana kuishi umri mkubwa iwezekanavyo kwa kutokustaafu na kuendelea kufanya kile unachopenda kufanya.

Rasilimali muhimu za kukusaidia kuishi miaka mingi.

Kama unataka kuishi miaka mingi iwezekanavyo, hakikisha unatumia rasilimali hizi;

1. Soma kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA uone jinsi ndani yako kulivyo na nguvu kubwa.

2. Soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA ili uweze kujenga biashara utakayoifanya maisha yako yote.

3. Soma kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA ili ianze biashara ukiwa kwenye ajira na unapostaafishwa kwa lazima uwe na kitu cha kuendelea kufanya.

4. Soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, ili uweze kuwa na akiba na uwekezaji wa kutosha, ili unapoishi miaka mingi uache kuwa tegemezi kwa wengine.

5. Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA ili kila siku usukumwe kuliishi kusudi lako na kupambania ndoto kubwa bila kuchoka wala kuridhika.

Kupata rasilimali hizo wasiliana na 0717 396 253.

Nikutakie maisha marefu sana rafiki yangu, maisha yenye tija kwako na kwa wengine wengi. Usikubali kufa haraka kabla ya muda wako, kila siku endesha mapambano ya mafanikio.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani
www.somavitabu.co.tz