Rafiki yangu mpendwa,
Nimewahi kukushirikisha siri moja kubwa ya kuishi miaka mingi ambayo ni kutokustaafu kazi.
Wote walioweza kuishi miaka mingi walikuwa bado wana kusudi na wajibu ambao unawasukuma kuendelea kuwa hai.
Huku wale wanaostaafu kazi zao kuona hawana tena wajibu hapa duniani, kitu kinachofanya wafariki mapema.
Kutokustaafu kazi ni sehemu muhimu ya kuishi miaka mingi. Lakini hiyo pekee haitoshi, kwani kama mtu unafanya kazi usiyoipenda au unayoifanya kwa mazoea tu na hutumii akili na ubunifu wako, unakuwa huna tofauti na aliyestaafu.

Aliyekuwa mwanamuziki bora kabisa kutokea nchini Hispania, Pablo Casals, ambaye aliweza kuishi miaka 97 huku akiendelea kufanya kazi yake mpaka siku anakufa, alikuwa na mengi mazuri ya kutushauri kuhusu kuishi miaka mingi.
Kwenye tawasifu yake aliandika;
“Katika kumbukizi ya kuzaliwa kwangu nilitimiza miaka 93, huo siyo umri mdogo, ni zaidi ya miaka 90. Lakini umri kwangu ni namba tu. Kama ukiendelea kufanya kazi na kufurahia uzuri wa dunia unagundua umri mkubwa haumaanishi kuzeeka. Nafurahia vitu sasa zaidi ya zamani na maisha yananivutia zaidi.”
Anaendelea kuandika;
“Kazi yangu ni maisha yangu, siwezi kufikiria kimoja bila ya kingine. Kustaafu kunamaanisha kuanza kufa. Mtu anayefanya kazi hachoki wala kuzeeka. Kazi na mapenzi kwenye vitu sahihi ni tiba bora ya uzee. Kila siku nazaliwa upya, kila siku naanza upya. Kwa miaka 80 iliyopita nimekuwa naianza kila siku yangu kwa mtazamo huo.” – Pablo Casals (December 29, 1876–October 22, 1973)
Rafiki, eneo la kuendelea kufanya kazi na kutokustaafu tumeshajifunza mara nyingi hapa.
Lakini Pablo ametuongezea kitu kipya, ambacho ni kuzaliwa upya kila siku, kuianza kila siku mpya kama ndiyo siku ya kwanza kwako.
Hebu jikumbushe siku ya kwanza kufanya chochote kile. Iwe ni siku ya kwanza kazini, kwenye biashara, mahusiano na mengine.
Siku ya kwanza huwa ni siku tunayoifurahia sana, siku tunayokuwa na hamasa na matumaini makubwa.
Hebu fikiria kama utayaishi maisha yako yote kama ndiyo siku ya kwanza kwako, kwa hakika yatakuwa maisha bora kabisa.
Hiyo ndiyo siri ya kuishi miaka mingi tunayojifunza kutoka kwa Pablo Casals, kuiishi kila siku kama siku ya kwanza kwako, hivyo kuweka juhudi kwenye kazi na kufurahia yale dunia inaleta kwako.
Hili linawezekana kwa kila mmoja wetu kuanza kufanyia kazi mara moja. Huna cha kusubiri, ni wewe kuamua kuyaishi maisha yako kwa namna hii na ikawa na manufaa makubwa kwako.
Ukaongeza miaka mingi na yenye tija kwenye maisha yako.
Usikubali kuziishi siku zako kwa mazoea, badala yake ikaribishe kila siku mpya kama siku ya kwanza kwako na iishi hivyo.
Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.somavitabu.co.tz
