2409; Mwanzo wa mwisho na mwisho wa mwanzo…
Rafiki,
Nataka kusema na wewe leo kuhusu kuanza.
Huwa kuna kauli ya Kiswahili inayosema mwanzo ni mgumu.
Lakini kwenye safari ya mafanikio hakuna kitu rahisi kama kuanza.
Najua ulishaanza mambo mengi mno, lakini hukuyafanya kwa muda mrefu.
Ni pale ulipokutana na ugumu ndipo ulikimbia na kwenda kuanza kitu kingine.
Mafanikio yako hayatokani na wingi wa vitu ulivyoanza, bali vile ambavyo umefanya mpaka kukamilisha.
Hivyo ili kufanikiwa, unapaswa kuwa na mwanzo wa mwisho na kisha mwisho wa mwanzo.
Mwanzo wa mwisho ni kuamua kuachana na kuanza mambo mapya kila wakati.
Badala ya kukimbizana na kila kitu kipya kinachopita mbele yako, weka juhudi kwenye kile ulichokwisha anza.
Mwisho wa mwanzo ni kuhakikisha kwa kila unachoanza unakifanya mpaka mwisho.
Usikimbie pale unapokutana na ugumu, badala yake uvuke ili uweze kupata mazuri.
Chochote rahisi kufanya huwa hakina thamani kubwa, kwa sababu kila mtu anaweza kukifanya.
Usitegemee urahisi kama unataka mafanikio makubwa, pale wengine wanapokutana na ugumu na kukimbia, wewe endelea kukomaa na kuweka juhudi.
Kuwa na mwanzo wa mwisho na fika mwisho wa mwanzo huo kabla hujawa na mwanzo mwingine.
Ushauri huu mfupi utaokoa sana muda na nguvu unazoweza kupoteza kwa kuhangaika na mengi.
Kocha.