2415; Zawadi na Adhabu…

Kituo kimoja cha kulelea watoto (day care) kiliona baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kuchelewa kuwachukua watoto wao.

Kituo hicho kikaamua kuweka adhabu ya faini kwa kila mzazi anayechelewa kumchukua mtoto wake.
Lengo la faini hiyo ilikuwa ni kuondoa hali ya wazazi kuchelewa.

Matokeo yakawa tofauti, badala ya wazazi kuwahi, wakawa wanachelewa zaidi na wengi kuliko awali.

Kwa nini?
Kabla ya kuwepo kwa adhabu, mzazi alijisikia vibaya alipochelewa. Lakini baada ya kuwepo kwa adhabu, kule kujisikia vibaya kukaondoka, hivyo hata anapochelewa hahangaiki asichelewe zaidi, badala yake anaenda akiwa ameandaa faini yake kabisa.

Serikali ya eneo moja huko nchini India iliona kuna tatizo kubwa la nyoka. Ikajaribu kila njia kuwatokomeza lakini hazikuzaa matunda.

Baadaye wakapata wazo la kuwatumia wananchi kutokomeza tatizo hilo. Serikali ikaanza kununua nyoka, kila mwananchi aliyepeleka nyoka alilipwa fedha.

Tatizo la nyoka liliisha, lakini cha kushangaza wananchi bado wakawa wanakuja na nyoka ili walipwe.
Serikali kuchunguza ikakuta kuna watu wanazalisha nyoka na kuwauza.
Hivyo watu wanaenda kununua nyoka hao kwa bei ya chini na kupeleka serikalini ambapo wanalipwa bei ya juu.

Mifano hiyo miwili ya uhalisia inatupa somo kubwa sana kuhusu zawadi na adhabu, tunapaswa kutumia njia hizo mbili kwa umakini mkubwa, la sivyo zinaweza kuleta madhara ambayo hukutegemea.

Adhabu zinaweza kuchochea zaidi kile unachotaka kukomesha, huku zawadi zikiondoa kile unachotaka kujenga.

Kila unapotaka kutumia zawadi au adhabu kama motisha, angalia namna gani zinaweza kuleta matokeo tofauti na unayotaka na kuzuia hilo lisitokee.

Binadamu ni wajanja sana, huwa wana tabia ya kuchezea mfumo wowote ule kwa namna ambayo utawanufaisha zaidi. Usipoweza kuziba kila aina ya mwanya, hutaweza kupata motisha unaotaka.

Kocha.