2416; Kuanzia chini ni kazi kubwa…

Mimi siyo mfuatiliaji wa michezo kabisa, lakini kama ambavyo nimekuwa nasema, kuna mambo utayasikia tu hata kama siyo mfuatiliaji wa habari.

Siku za hivi karibuni kumekuwa na mivutano kwenye timu kubwa za mpira Tanzania, hasa timu ya Simba ambapo kuna migogoro mbalimbali ya ndani.

Sasa niliona watu wakiwa wanabishana, wakisema kama mtu ni tajiri mkubwa, kwa nini asiende kuanzisha timu yake akaiendesha anavyotaka yeye badala yake anakuja kuhangaika na timu kongwe na kusumbuliwa?

Kuna mengi yako nyuma ya hilo, lakini jibu la wazi na la haraka ni hili; kuanzia chini siyo rahisi, hasa kujenga wafuasi au mashabiki wa kweli.

Unaweza kuwa na fedha nyingi utakavyo, lakini kuweza kutengeneza mashabiki na wafuasi wa kitu, wakipende kweli kutoka ndani ya mioyo yao, wawe tayari kujitoa kweli kwa ajili ya kitu hicho ni jambo linalohitaji muda. Muda mrefu sana.

Sasa kwa kuwa mtu hana muda mrefu wa kujenga hilo, na kwa kuwa anataka uwekezaji wake ulipe mapema, anakwenda pale ambapo tayari ushabiki wa kweli umeshajengeka.

Nataka unifunze nini hapa?
Weka muda na nguvu kwenye kutengeneza wafuasi na mashabiki wa kweli kwenye chochote kile unachofanya.

Hiyo ni mali (asset) ambayo baadaye utavuna manufaa makubwa na kwa muda mrefu.
Wakati unajenga utaona kama hakuna kinachofanyika, lakini siku itafika unashangaa ulichojenga kinakua chenyewe na kukunufaisha zaidi.

Kwenye kila unachofanya, usifanye tu kwa juu juu kama unakimbizwa, zama ndani na jenga mashabiki na wafuasi wa kweli.
Watu ambao wanaipata thamani kweli, wananufaika nayo na wapo tayari kujitoa zaidi kwa ajili ya hicho walichokiamini.

Hili linawezekana kabisa, ila linahitaji muda, uvumilivu na ung’ang’anizi.
Jenga wateja waaminifu kwako na kwa biashara yako, ambao siyo wa kuhama hama kila mara.
Hiyo ni mali ambayo ukiijenga kwenye chochote unachofanya, utakuwa msingi bora na imara kwa mafanikio yako makubwa kwenye kitu hicho.

Kocha.