2418; Kwa sababu maisha yako yote yanategemea hapo…

Huwa tunakipa kitu uzito kulingana na namna kinavyoathiri maisha yetu moja kwa moja.

Kama maisha yanategemea zaidi kitu fulani, basi tunakipa kitu hicho kipaumbele cha kwanza.

Ndiyo maana kwenye dharura, watu huwa tayari kufanya chochote ili tu kuokoa uhai wao.

Hivyo basi, kama kuna kitu ambacho unataka kufanikiwa na kufanya makubwa, yafanye maisha yako yakitegemee sana kitu hicho.

Chukua mfano wa biashara, kwa mtu ambaye hana kingine cha kutegemea ila biashara, atajituma sana kwenye biashara hiyo.
Lakini kwa ambaye anafanya biashara kama kitu cha pembeni tu, hatajisukuma sana.

Kwa maana nyingine ni huwezi kupata mafanikio makubwa kwenye kitu ambacho siyo kipaumbele cha kwanza kwako.
Kama hujayaweka maisha yako rehani, kwamba yategemee sana kwenye kitu, kuna namna tu utazembea na hilo litakuwa kikwazo.

Hapa ndiyo tunajifunza kupitia hadithi ya mkuu wa kikosi aliyevuka na wapiganaji wake mpaka ng’ambo ya pili ya maji, kisha kuchoma moto vyombo walivyotumia kuvuka, akiwaambia wanapaswa kupambana washinde au wafe, hakuna kurudi nyuma.
Kwa hilo mtu anajua kabisa maisha yake yanategemea yeye kushinda, la sivyo anapotea, kitu kinachomsukuma zaidi.

Ni maeneo gani ya maisha yako umekuwa unasua sua kupiga hatua lakini ni maeneo muhimu kwa mafanikio yako?
Yafanye maisha yako kutegemea kwenye maeneo hayo na utashangaa jinsi utakavyoweza kubadilika kwa kasi kubwa.

Mhamasishaji Erick Thomas amekuwa anasema hakuna mtu mvivu duniani, wale tunaoona ni wavivu ni kwa sababu maisha yao hayajawa rehani. Anasema mchukue mtu unayeona ni mvivu kabisa, mpeleke kwenye kina kirefu cha maji kisha mzamishe kwa nguvu.
Ghafla utashangaa mtu anapata nguvu ya ajabu ya kupambana na wewe na kujiokoa asife.

Maisha yako yakitegemea kwenye kitu, utakipa kipaumbele cha kwanza na kuweza kufanikiwa sana kwenye kitu hicho.

Kocha.