2420; Kuna watu wananufaika hata kama hawakuambii…
Tatizo kubwa kwenye maisha, hasa kwenye safari ya mafanikio ni upweke utakaokutana nao.
Mara kwa mara utajikuta kwenye hali ya upweke, ukijiona uko mwenyewe kwenye mapambano unayoendesha.
Katika nyakati hizo ndiyo mawazo ya kukata tamaa hukujia, yakikushawishi kwamba hakuna anayejali.
Lakini mimi nataka nikuambie kitu kimoja, kuna watu wanakufuatilia na kunufaika na unachofanya, hata kama hawakuambii moja kwa moja.
Wapo wanaonufaika na matokeo ya kile unachofanya, hivyo unapoacha kufanya unawanyika kile wanachonufaika nacho.
Na muhimu zaidi, wapo watu wanapata moyo kwa kukuona wewe ukifanya unachofanya, kwa sababu unawaonyesha kwamba inawezekana, kitu ambacho hawajawahi kuona.
Kila unapojiona mpweke kwenye hii safari ya mafanikio, jua ni fikra na hisia zako tu zinakudanganya.
Kuna wengi wapo na wewe, japo wengi hao hawajionyeshi wazi.
Hili halimaanishi kwamba ufanye kwa ajili ya wengine, bali kabla hujakata tamaa, jua ni wangapi utawaathiri na kuwakatisha tamaa pia.
Maana wajibu wetu siyo tu kupata kile tunachotaka sisi, bali kuwawezesha wengine pia wapate kile wanachotaka.
Kupitia chochote unachofanya, kuna namna unawasaidia wengine kupata wanachotaka.
Safari ya mafanikio ni ngumu na inayoonekana kuwa ya upweke, lakini jua kuna wengi walio nyuma yako kuliko unavyoona.
Jikumbushe hili mara zote.
Kocha.