2426; Kusikia na kuona…

Kama unachosikia kinatofautiana na unachoona, amini kile unachoona.

Uongo huwa ni rahisi sana kusemwa, lakini ni mgumu kuonyeshwa.

Kwenye kila aina ya uongo, huwa kuna ukweli unaoonekana wazi, lakini kwa sababu tunataka sana kusikia kile tunachotaka, tunaishia kudanganywa.

Ni vigumu sana kudanganywa kama macho yako yatakuwa wazi na kuviona vitu vilivyo badala ya kupigwa upofu na kile unachosikia.

Hata katika hali ya ana kwa ana, mtu anaweza kudanganya kwa mdomo, lakini macho yakaweka wazi, lugha ya mwili ikatoa ukweli wote.

Na hapo bado hujatumia machale yako, ambayo pia huwa yanaona na kuhisi kwa haraka kabla hata hujaelewa nini kinachoendelea.

Waongo hawataisha, wenye nia ya kujifaidisha kupitia wewe wataendelea kuwepo. Umakini wako ndiyo unaokuwa silaha kwako kuepuka kudanganywa na kutapeliwa.

Sasa kwa zama hizi tunazoishi sasa, zama ambazo umakini wa watu umekuwa mdogo sana, kazi ya walaghai na matapeli imekuwa rahisi.

Wewe usikubali kuwa windo rahisi kwa watu wako, weka umakini wako juu na utaona ukweli kama ulivyo, hata kama unafichwa kiasi gani.

Kocha.