Rafiki yangu mpendwa,
Imeandikwa kabisa kwamba ijue kweli nayo itakuweka huru.
Watu wengi hawapo huru kwa sababu hawataki kuuangalia na kuupokea ukweli.
Na hiyo ni kwa sababu ukweli huwa unaumiza.

Inapokuja kwenye swala la fedha, kutokuujua ukweli imekuwa chanzo cha maumivu makubwa kwa wengi kifedha.

Leo kuna ukweli kuhusu fedha nataka nikuambie, ambao ukiuelewa, japo utakuumiza, lakini pia utakuweka huru.

Kuna kichekesho nimekuwa naona kinazunguka mtandaoni.
Mtu amepiga magoti anasali, anamwomba Mungu amkopeshe mamilioni ya fedha, kwani Mungu anajua mtu huyo hana pa kukimbilia na anajua atakuwa hapa duniani kwa muda gani.

Japo ni kichekesho, lakini kuna ujumbe ambao uko nyuma yake. Kwamba wanachofikiri wengi kwenye fedha ni wanazikosa kwa sababu hawajapewa kile wanachostahili.
Na hapo ndipo wengi wanapokosea, hupati fedha kwa sababu unastahili.

Haina tofauti na mwanafunzi wa darasa la saba, aende kwa mwalimu na kumuomba ampe mtihani wa darasa la saba afanye, kwa sababu atakuwa hapo shuleni mpaka darasa la saba.
Swala siyo muda au uwepo, swala ni uwezo wa kuhimili jambo.

Unakosa fedha siyo kwa sababu hustahili, ila kwa sababu huwezi kuzimudu.

Huwa kuna kauli kwamba benki ni taasisi inayokupa fedha pale unapoithibitishia kwamba huhitaji fedha hizo.
Yaani ili benki ikupe mkopo, lazima uithibitishie kwamba unaweza kulipa mkopo huo, kwa kuwa na mali au kipato cha uhakika.

Unaona hapo rafiki, kama benki zingekuwa zinatoa fedha kwa sababu watu wanastahili kuzipata, masikini wote wanastahili. Lakini wakipewa hizo fedha hawawezi kuzimudu, hivyo benki zingeishia kupata hasara.
Hivyo cha kwanza ambacho benki inataka ni kujua kama mtu anaweza kumudu fedha ambazo inampatia.

Unataka mkopo wa milioni 10 wakati huna hata kitu cha milioni moja! Benki inajua kabisa huwezi kumudu kiasi hicho na hivyo haikupi. Unataka mkopo wa milioni 10 wakati una nyumba ya milioni 20, hapo benki inakupa, kwa sababu inajua utaweza kuimudu fedha hiyo.

Rafiki, ukweli kuhusu fedha siyo kustahili ni kumudu.

Tukirudi kwenye kichekesho nilichoanza nacho hapo juu, vipi kama Mungu akiamua kumjibu muombaji, akimuuliza fedha zote nimewahi kupitisha kwenye mikono yako una nini cha kuonyesha?
Nina hakika hapo muombaji atabaki mdomo wazi.

Rafiki, hebu jiulize hilo, kama labda umefanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 na huna hata milioni moja umeweza kuweka kama akiba, hivi unadhani tatizo ni fedha na kazi unayofanya au tatizo ni wewe?

Ukiwa hutaki kuukabili ukweli, utatafuta kila aina ya kisingizio. Lakini kama upo tayari kwa ukweli ambao utakuweka huru, lazima utaona wapi unapokosea na kujirekebisha.

Ninachotaka kukueleza hapa rafiki yangu ni hiki, kama kuna kiwango cha fedha unakihitaji lakini hujakipata, tatizo siyo kwamba umenyimwa au hustahili, tatizo ni kwamba bado hujathibitisha unaweza kumudu kiasi hicho cha fedha.

Na unaweza kuthibitisha hilo kwa namna unavyomudu kiasi kidogo cha fedha kinachopita kwenye mikono yako.
Anza sasa kumudu kila fedha inayopita kwenye mikono yako.
Jiwekee tozo zako mwenyewe, kwa kila pesa inayopita kwenye mikono yako, asilimia kumi inapasea kuwa TOZO YA KUJILIPA WEWE MWENYEWE KWANZA.

Kama ambavyo serikali inaweka kila aina ya tozo kwenye fedha yako, jiwekee na wewe tozo pia, ambayo itakuja kukuondoa hapo ulipo kifedha.

Rafiki, kujifunza zaidi jinsi unavyoweza kujijengea kumudu kiwango kikubwa cha fedha, pata na usome kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA. Kukipata kitabu hiki wasiliana na 0752 977 170.

Kwenye kitabu hicho nimeelezea kwa kina dhana ya KIPIMA JOTO CHA KIFEDHA, dhana inayokupa uelewa kwa nini ukipata fedha nyingi kuliko ulivyozoea unaishia kuzipoteza.
Ndiyo hili la kumudu tulilojifunza hapa leo.
Jifunze hilo kwa kina kwenye hiyo dhana ya kipima joto, ili uwese kupandisha kiwango chako cha kifedha na upate zaidi ya unavyopata sasa.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
www.somavitabu.co.tz