2428; Mafanikio yako ni hatari kwa wengine…

Kabla hujafanikiwa, watu wanakuchukulia poa.
Kwanza wanajua hutaweza kufanikiwa sana, hivyo huwi hatari kwake.

Unapofanikiwa kwa viwango vya juu na kuwapita wao kimafanikio, ghafla wanabadilika na kuanza kuwa kikwazo kwako.

Wanafanya hivyo kwa sababu wanakuona wewe ni hatari kwao, na hatari hiyo inatokana na mambo mawili.

Moja wanaona hawawezi tena kukutumia kama kipindi cha nyuma. Kabla hujafanikiwa walikuwa wanaweza kukutumia kwa manufaa yao. Labda kukutaka uwafanyie kazi fulani ambazo hazina maslahi kwako.
Sasa unapofanikiwa hilo haliwezekani tena, hivyo wanakosa kile walichozoea.

Mbili ni mafanikio yako yanawafanya wao waonekane ni wazembe. Kwa sababu wakati unaanzia chini wao walikuwa juu tayari na sasa umekwenda juu kuliko wao, unafanya waonekane ni wazembe na hawawezi kutoa kisingizio kwa nini hawajafanikiwa zaidi.
Hivyo kuwa kikwazo kwako ndiyo njia yao ya kuficha uzembe wako.

Kwa kujua hili muhimu, unapaswa kulitumia kwa njia mbalimbali.

  1. Kujua siyo watu wote watakaofurahia mafanikio yako, na kwa hakika, wengi mno hawatafurahia wewe kufanikiwa.
    Tukiuweka ukweli kama ulivyo kuna watu wachache mno ambao wanaweza kuyafurahia mafanikio yako makubwa.
    Wengi kuna kiwango cha mafanikio ukifikia wanajikuta tu wanaingiwa na wivu.
    Hiyo ni asili ya binadamu.

  2. Kadiri unavyozidi kufanikiwa ndivyo unavyopaswa kutokuweka mambo yako mengi hadharani. Unapokuwa unaanzia chini, unahamasika kushirikisha hatua unazopiga, maana zinakupa hamasa na zinawapa wengine hamasa pia.
    Lakini unapaswa kujua kadiri unavyopiga hatua, ndivyo unavyoibua wivu kwa wengi. Hivyo shirikisha wachache sana mafanikio yako halisi, wengine acha wadhanie tu.

  3. Ukishamjua mtu ambaye hayafurahii mafanikio yako, usiumie wala kujaribu kumbadili, badala yake kaa naye mbali. Hakikisha humpi mtu huyo nafasi ya kukuletea madhara au kuwa kikwazo kwako.

Unapopambana kufanikiwa, usisahau wapo watu watakaopambana kukuangusha.
Jiandae kwa hilo ili lisiwe kikwazo kwako.

Kocha.