Rafiki yangu mpendwa,
Tafiti za kisaikolojia zimekuwa zinaonyesha kwenye mashindano yoyote yale, kushinda au kushinda huwa kunaanza kabla hata ya pambano.
Yaani pambano la mwisho siyo linaloamua mshindi, bali linamuonyesha mshindi.
Mshindi na mshindwa wanakuwa wameshapatikana kabla hata hawajaingia kwenye pambano.
Na hilo linaanzia kwenye fikra. Yule anayeenda kwenye pambano akifikiria kitu kimoja tu, yaani ushindi, kwa kila namna atashinda.
Lakini yule anayeenda akifikiria uwezekano wa kushindwa, ataishia kushindwa.
Washindi ni wale ambao msamiati wa kushindwa haujawahi kuwepo kwenye fikra zao. Hawajui kitu kinachoitwa kushindwa.
Wao wanachojua ni kupambana na kushinda.
Kwa mtazamo wa aina hiyo, unajionea wazi kwa nini baadhi ya watu wanafanikiwa hata iweze.
Na kama unataka mafanikio makubwa kwenye maisha yako, lazima na wewe ujijengee mtazamo wa aina hiyo, mtazamo wa kwamba hakuna kitu kinachoitwa kushindwa, bali kuna kupambana na kushinda tu.

Rafiki, kwenye biashara pamoja na huo mtazamo, kuna kitu kingine kinachoamua kama biashara itafanikiwa au itakufa.
Na kitu hicho kinakuwepo kabla hata ya biashara kuanza.
Yaani biashara inafanikiwa au kushindwa kabla hata haijaanzishwa.
Na hili ni muhimu sana kulijua kwa sababu limekuwa kikwazo kwa biashara nyingi kushindwa.
Biashara nyingi changa huwa zinaingia kwenye changamoto na kushindwa kwa sababu zinaanzishwa kwa mtazamo usio sahihi.
Mtazamo wa biashara huwa unatokana na swali ambalo mwanzilishi wa biashara anajiuliza.
Kuna maswali mawili ya kujiuliza;
Moja, ni biashara gani itakayoniwezesha kupata fedha ya kuendesha maisha?
Mbili, ni biashara gani inayonipa nafasi ya kumhudumia mteja vizuri kuliko anavyohudumiwa sasa?
Maswali hayo ni rahisi lakini yamebeba maana kubwa na yana hatima ya kushinda au kushindwa kwa biashara yako.
Unapoanza biashara kwa msingi wa swali la kwanza, unaangalia ni kwa namna gani wewe utanufaika.
Unakazana kuangalia biashara yenye faida kubwa na isiyokusumbua.
Kwa sehemu kubwa biashara ya aina hiyo haipo na hivyo utajikuta unahangaika na kila aina ya biashara na usifanikiwe.
Usisahau pia kipindi cha mwanzo cha biashara yoyote ile huwa hakuna faida na changamoto ni nyingi.
Hivyo kama umeingia kwa msukumo wa kupata faida tu, hutaweza kudumu kwenye biashara hiyo, kwa sababu kilichokupeleka hukioni.
Hii ndiyo sababu ya watu kuhangaika na kila fursa mpya wanayosikia ya biashara, kwa kuona ni nafasi ya kupata faida kubwa na ya haraka bila ya kuweka kazi.
Unapoanza biashara kwa msingi wa swali la pili, unatafuta changamoto ambayo watu wanayo na kisha unaitatua kwa namna bora kuliko inavyotatuliwa kwa sasa.
Unachagua aina ya wateja ambao utawahudumia vizuri sana, kwa namna ambayo hawajaweza kuhudumiwa mpaka sasa.
Hapo unayaweka maslahi ya wateja wako mbele na kuhakikisha wananufaika kweli.
Kwa njia hii ya pili, unatoa thamani kubwa, thamani ambayo wateja hawawezi kuipata sehemu nyingine yoyote.
Hili linaleta matokeo makubwa sana baadaye.
Wateja wanaopata thamani wataendelea kuwepo kwenye biashara kwa sababu wananufaika.
Lakini zaidi watawaleta wateja wengine kwa sababu watakuwa mashuhuda wazuri wa biashara yako.
Japo njia ya pili itachelewa kukupa faida, maana hutaingiza faida kwa haraka. Lakini ndiyo njia ambayo itakuja kukupa faida kubwa na ya kudumu kwa muda mrefu.
Biashara inashinda au kushindwa kutokana na swali ambalo mwanzilishi anajiuliza kabla hata hajaingia kwenye biashara.
Kama unaingia kwenye biashara kwa sababu unataka faida kubwa, ya haraka na isiyokusumbua, biashara inakwenda kushindwa.
Lakini kama unaingia kwenye biashara kwa sababu kuna changamoto umeona watu wanayo na unaweza kuitatua vizuri kuliko inavyotatuliwa sasa, utajenga biashara ambayo itadumu kwa muda mrefu na kuzalisha faida kubwa.
Kama upo kwenye biashara, ni swali lipi unalofanyia kazi kati ya hayo mawili?
Kama unapanga kuingia kwenye biashara ni swali lipi linakusukuma kati ya hayo mawili?
Usikose kusoma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA ili uweze kujifunza namna ya kutoa thamani kwa wateja wako na upate faida nzuri. Kupata kitabu wasiliana na 0752 977 170.
Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.somavitabu.co.tz
