2429; Wa mwisho kwako, wa kwanza kwake…
Kitu kimoja kikubwa ambacho najifunza kwenye taaluma ya udaktari ni mitazamo tofauti ambayo daktari na mgonjwa wanakuwa nayo.
Kama daktari unaweza kuwa kwenye zamu ya kuona wagonjwa na umekaribia mwisho kabisa wa zamu yako, umechoka na anakuja mgonjwa wa mwisho.
Wewe daktari unaweza kumuona huyu ni mgonjwa wa mwisho, wacha nimalizane naye haraka haraka na niondoke.
Lakini mgonjwa anapokuja kwako anajiona yeye ni wa kwanza kwako. Hajali umeona watu wangapi kwenye zamu yako, yeye anajijua ana shida na anataka kipaumbele cha kwanza.
Na tofauti hii ya kimtazamo ndiyo imekuwa chanzo cha huduma kutokuwa nzuri na wateja kutokuridhika na namna walivyohudumiwa.
Hili tunaweza kulitumia kwenye kazi na biashara zozote tunazofanya ambazo tunakutana na wateja.
Kamwe usimchukulie mteja yeyote kama wa mwisho na kumpa huduma za juu juu.
Badala yake mchukulie kila mteja kama wa kwanza na mwenye uhitaji mkubwa.
Mpe umakini wako wote.
Mfanye kuwa kipaumbele cha kwanza kwako.
Japo wateja wanaweza wasikuambie, lakini wanajua wazi pale unapokuwa umewahudumia kwa kujali au kwa haraka bila kujali.
Na kwa zama hizi, wateja wanakuadhibu kwa kuchagua kwenda kupata huduma mahali pengine ambapo wanajaliwa kweli.
Jikumbushe hili mara zote unapowahudumia wateja ili kutoa huduma bora.
Na pia ufanye huu kuwa msingi wa biashara yako, kila anayehusika na wateja, basi awape huduma bora kabisa.
Ni mambo madogo madogo ambayo ni rahisi kuyapuuza ndiyo yanayojenga au kubomoa biashara. Zingatia kila kinachohusika kwenye biashara yako.
Kocha.