Rafiki yangu mpendwa,
Karne ya 19 na ya 20 zilikuwa karne za maendeleo makubwa mno duniani.

Ndiyo kipindi ambacho teknolojia nyingi mpya ziligunduliwa na matatizo mengi ya binadamu kutatuliwa.

Kwa namna mambo yalivyokuwa yanaenda kwa kasi, walioishi kipindi hicho walijua mpaka kufika karne ya 20, binadamu tutakuwa tumepiga hatua kubwa mno.

Walitegemea umri wa watu kuishi uwe mrefu, safari za kwenda angani na kwenye sayari nyingine kuwa kitu cha kawaida na changamoto nyingi kupata majibu.

Karne ya 21 ikaingia, kasi ya teknolojia ikawa kubwa hasa baada ya kusambaa kwa mtandao wa intaneti.

Lakini cha kushangaza, kasi ya maendeleo ya teknolojia na utatuaji wa changamoto ikapungua sana.
Japo upande wa TEHAMA umekua unaendelea kwa kasi, maeneo mengine hayana kasi ya aina hiyo.

Na hapo ndipo tatizo kubwa linapoanzia, maendeleo makubwa kwenye sekta ya TEHAMA, yamekuwa kikwazo kwa maendeleo ya sekta nyingine.

Hiyo ni kwa sababu sekta ya TEHAMA imetuletea teknolojia ambazo zinatupa usumbufu mkubwa na kupoteza muda wetu mwingi.

Chukua mfano wa simu janja, simu yenye uwezo mkubwa tunayotembea nayo kila mahali. Mara nyingi kifaa hicho kimekuwa ni usumbufu. Ni vigumu mtu kupata muda tulivu wa kufanya kazi zenye tija.

Angalia mitandao ya kijamii, ambayo ni mingi na kila siku inaongezeka. Mitandao hiyo imekuwa kazi ya ziada kwa watumiaji, huku ikiwa haina tija kwenye kazi muhimu ambazo mtu anafanya.

Mitandao ya kijamii imekuwa inaleta raha ya haraka, kitu kinachowafanya watu kuwa wateja wa mitandao hiyo.
Pale mtu anapokuwa amechoshwa na kazi anayofanya au kukutana na ugumu, badala akomae hapo, anakimbilia kwenye mitandao.

Hilo linaathiri sana ubunifu, kwani tafiti zinaonyesha watu huwa na ubunifu pale wanapokuwa kwenye hali ya uchoshi au kukutana na ugumu ambao wanapambana nao kwa muda mrefu.

Tatizo ni kwenye hizi zama, unapofanya kazi na kukutana na ugumu, unakimbilia kwenye mitandao ya kijamii badala ya kupambana na ugumu huo.
Hilo linapunguza ubora wa kazi na kushusha ubunifu pia.

Tufanye nini ili kuondokana na hali hii?
Jibu lipo wazi, tunapaswa kudhibiti sana matumizi yetu ya simu janja na mitandao ya kijamii.

Usikubali simu yako ikutawale wewe, kwa kuwa usumbufu kwako masaa 24 ya siku na siku saba za wiki.

Kwenye kila siku yako tenga muda usiopungua masaa mawili ambapo utafanya kazi zako kwa utulivu na ufanisi wa hali ya juu sana.

Unapokutana na ugumu au uchoshi, usikimbie,  bali baki hapo kwenye kazi yako kwa muda uliotenga.

Ni katika nyakati hizo ndiyo akili yako inajisukuma na kuja na majibu ya tofauti, majibu yanayochochea ubunifu wako.

Najua unaweza kuwa unajiambia huwezi kukaa mbali na simu yako kwani ndiyo kila kitu kwako.

Lakini nikuambie tu, kama huwezi kupata angalau masaa mawili ya kufanya kazi yako bila ya usumbufu wowote ule, unachofanya ni zimamoto.

Na zimamoto huwa haileti matokeo yoyote mapya. Utajiona unahangaika sana ila hakuna hatua zozote kubwa unazokuwa umepiga.

Kujifunza zaidi jinsi ya kuondoka kwenye utumwa wa teknolojia mpya, ili uweze kuwa na udhibiti wa fikra zako na kufanya makubwa, soma kitabu cha EPUKA UTUMWA WA KIDIJITALI.

Hiki ni kitabu kinachokuonyesha jinsi teknolojia mpya zinavyojenga uraibu kwako na kuteka fikra zako kiasi kwamba huwezi kupata utulivu wa kufanya mambo ya maana.
Lakini pia kinakupa suluhisho la uhakika, ambalo linakuwezesha kurudisha uhuru wako na kufanya makubwa.

Kama bado hujasoma kitabu hiki, kipate leo na ukisome. Wasiliana na 0752 977 170 kujipatia nakala yako ya kitabu leo.

Teknolojia ina fursa ya kutuwezesha kufanya makubwa, lakini pia ina hatari ya kutufanya watumwa.
Kuzitumia teknolojia kwa mazoea ni hatari kubwa kwako.
Pata maarifa sahihi sasa ili uzitumie teknolojia vizuri.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
www.somavitabu.co.tz