2430; Unaona kile unachotaka kuona…

Sisi binadamu kwa kujidanganya huwa tupo vizuri sana.

Ila huwa hatujui kama tunajidanganya, tunakuwa na ukakika tumesimama kwenye ukweli.

Ila ni mpaka pale uzio ulio kati ya ukweli na uongo unapoanguka ndiyo tunaona wazi tulikuwa tunajidanganya.

Huwa tunaona kile tunachotaka kuona na kukusanya ushahidi unaoendana nacho, huku tukificha ushahidi unaopingana nacho.

Tunakuwa na uhakika sana kwamba tutapata kile tunachotaka na hata ushahidi unapokuwa mbele yetu kamba tunaweza tusipate, huwa hatuuoni kabisa.

Hili ndiyo hupelekea watu kuja kuona kama walilogwa au kuwekewa dawa na wakawa hawaoni ukweli.

Chukua mfano wa mapenzi. Labda mtu amekutana na mtu mwingine, wakapendana sana na wakapenda sana kuwa pamoja.

Watu hao, hawawezi kuona madhaifu yaliyo kwa wenzao na hata wao wenyewe ambayo yanaweza kuwa kikwazo kwao.

Na hata pale wengine wanapowashauri kulingana na madhaifu wanayoyaona, huwa hawawasikilizi, badala yake wanaona wanawaonea wivu kwa namna wanavyopendana.

Lakini pale madhaifu hayo yanapokuja kutengeneza changamoto kubwa na watu hao wakashindwa kuendelea pamoja ndiyo mtu anaona kama amefumbuliwa macho.

Anaona mengi ambayo hakuweza kuyaona awali na hapo ndipo anapoamini alilogwa au kuwekewa madawa.

Kumbe uchawi wake ni yeye mwenyewe, kutaka sana kitu kiasi kwamba anakuwa na upofu kwa kitu kingine ambacho ni tofauti na anachotaka.

Kuvuka udhaifu huu ambao kila mmoja wetu anao, lazima tuangalie upande hasi wa kila jambo.

Hata kama ni kitu unapenda sana kiwe kwa namna fulani. Hata kama ni kitu ambacho una uhakika ndiyo unachotaka na utakachopata.
Jiulize vipi kama kikiwa tofauti?

Pata picha hujakipata au kimekuwa tofauti na ulivyotegemea.
Je itakuwaje?
Je utaendeleaje?

Hayo ni maswali muhimu ya kujiuliza na kujijibu ukiwa na utulivu mkubwa ili uweze kuuona ukweli halisi na siyo kile unachotaka kuona wewe.

Kujidanganya ni rahisi na kunabembeleza, ila maumivu yake ni makubwa baadaye.
Bora uukabili ukweli mapema na ukuumize, kuliko kujibembeleza na ukweli na kuja kuumia zaidi baadaye.

Kocha.